Mourinho alilia kurudi mzigoni

Tuesday August 20 2019

Mourinho alilia, kurudi mzigoni, Mwanaspoti, Tanzania, Michezo, Mwanasport

 

LONDON, ENGLAND. JOSE Mourinho amesema kwa masikitiko kwamba amemisi kuwa kocha huku moja ya mastaa wake aliowahi kuwanoa huko nyuma akimwambia arudi haraka kuja kuwanyoosha!
Mourinho, aliyejipachika jina la The Special One, amekuwa hana kazi tangu Desemba mwaka jana wakati alipofutwa kazi huko Manchester United na nafasi yake kuchukua Ole Gunnar Solskjaer. Kocha huyo Mreno alisema kwa sasa anachokiwaza ni kurudi kwenye kazi yake ya ukocha kabla haujapita muda mrefu sana.
Mourinho alisema: "Nilienjoi sana. Kipindi kile nilipoingia kwenye soka la kulipwa, kipindi ambacho niliwashika. Na sasa imekuwa siriazi, kazi siriazi. Lakini sasa nimesimama, badala ya kufurahia, sienjoi tena, nimemisi sana."
Tangu afutwe kazi Old Trafford, Mourinho ameamua kuingia kwenye kazi ya uchambuzi wa soka kwenye televisheni ya Sky Sports na kudai kwamba anasubiri kazi ya maana zaidi baada ya kugomea ofa ya kwenda China. Ni miezi minane sasa tangu awe hana kazi ya ukocha ikiwa ni muda mrefu kama ilivyowahi kutokea huko nyuma alipoondoka Chelsea, Septemba 2007 na kwenda kujiunga na Inter Milan Juni 2008.
Kiungo Cesc Fabregas, aliyewahi kushinda ubingwa wa Ligi Kuu England akiwa chini ya Mourinho huko Chelsea, amemtaka kocha huyo kurudi tena kwenye kazi yake ya ukocha.
Kiungo huyo Mhispaniola alisema: "Gwiji. Tumekumisi. Rudi haraka bwana."
Mashabiki wengi wa AS Monaco wanamtaka Mourinho aende akamrithi Leonardo Jardim kwenye kikosi chao baada ya kuona timu inafanya hivyo kwenye Ligue 1, ambapo timu hiyo imepoteza mechi zote mbili za mwanzo kwenye ligi hiyo msimu huu.

Advertisement