Shiboub, Chilunda ni shoo ya kibabe

Monday August 19 2019

Shiboub, Chilunda ni shoo ya kibabe, Simba, Azam, Mwanaspoti, Tanzania, Michezo

 

By THOMAS NG’ITU

Dar es Salaam. ULE ubishi wa nani zaidi kati ya Simba na Azam umemalizwa kibabe. Ndio, ni juzi tu hapo Uwanja wa Taifa, wakati Wekundu wakitakata mbele ya Wanalambalamba kwa kuwapa kipigo cha mabao 4-2.

Hicho kilikuwa kipigo cha pili kwa Azam mbele ya Simba kwenye michuano hiyo iliyoasisiwa mwaka 2001 na kusimama kabla ya kurejeshwa tena 2009.
Pia ni mechi ya kwanza iliyozalisha mabao mengi ikiupiku mchezo wa awali wa timu hizo mwaka 2012 walipofungana mabao 3-2, Azam ikilala tena.
Sasa achana na utamu wa ushindi huo wa Simba, unaambiwa burudani ya mchezo huo wa 12 wa michuano hiyo, ni soka la kuvutiwa lililopigwa na kiungo Shiboub Sharaf Eldin, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Hassan Dilunga ‘HD’ kwa Simba na lile la Shaaban Idd Chilunda, Frank Domayo na Salum Abubakar ‘Sure Boy’.
Hata mabao yaliyofungwa na Shiboub, Chama, Kahata, Chilunda na Domayo yote yalikuwa bab’kubwa mbali na udambwidambwi uliotawala dakika 90 za pambano hilo na Mwanaspoti iliyokuwa uwanjani inakuchambulia mchezo mzima ulivyokuwa.

SIMBA, AZAM FIFTE FIFTE
Katika mchezo wa jana ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza, Simba walionekana kumiliki mpira na kutengeneza mashambulizi kupitia pasi nyingi huku Azam wakitumia mipira mirefu.
Mipira mirefu ambayo walikuwa wakitumia Azam ilikuwa na faida kutokana na washambuliaji wao Chilunda na Dally Ella Djodi walikuwa wepesi katika kuipata mipira hiyo na kuwasumbua mabeki wa Simba.
Kipindi cha pili mambo yalikuwa fifte fifte, huku Azam wakifanya mambo kipindi cha pili licha ya kuzidiwa na wapinzani wao ambao ndio Mabingwa wa Tanzania katika Ligi Kuu.

KAKOLANYA SAFI
Katika kipindi cha kwanza kipa Kakolanya alionyesha umahiri mkubwa wa kuwapanga mabeki wake Pascal Wawa na Erasto Nyoni licha ya kwamba walikuwa wakikatika mara kwa mara.
Kakolanya aliweza kuokoa michomo miwili katika kipindi cha kwanza baada ya dakika 7, kiungo Salum Abubakar kupiga pasi mpenyezo kwa  Chilunda ambaye alibaki na kipa lakini alipouinua mpira juu ya kipa aliyekuwa amevutika mbele, mpira haukurudi chini, ukapita juu la lango.
Chilunda alipata nafasi nyingine ya wazi dakika 30 baada ya kubaki yeye na Kakolanya uso kwa uso lakini kipa huyo alitokea na kupunguza goli na kumfanya Chilunda asijue chakufanya.
Kwa upande wa kipa Razack Abarola wa Azam, alikuwa mzuri wa kuchomoa mikwaju ya washambuliaji wa Simba, lakini kupishana kwa maelewanao kati ya Oscar Masai na Yakub Mohammed kuliwagharimu Azam.
Abarola alijitahidi kuwapanga kila alivyoweza lakini hilo halikusaidia kwani Simba walikuwa wakizidisha mashambulizi wakitumia mipira ya pembeni kwa mabeki Kapombe na Tshabalala. Kosa lake la kupangulia ndani shuti kali la Hassan Dilunga ‘HD’, liliwazadia Simba goli lililofungwana Shiboub.

WAWA, NYONI BADOBADO
Maelewano ya mabeki wa Simba, Erasto Nyoni na Pascal Wawa bado hayajawa fiti kutokana na wachezaji hawa kupishana mara kwa mara.
Katika kipindi cha kwanza walionekana kukatika na kiungo Sure Boy alikuwa akipenyeza mipira kwa Chilunda ambaye alikuwa mwiba katika kipindi cha kwanza.
Hali hiyo iliwafanya Azam kupata bao dakika 13 baada ya Chilunda kupiga shuti kali na kumuacha kipa Beno Kakolanya akikosa la kufanya.
Katika kipindi cha pili walionekana kuanza kuelewana, lakini Azam nao walifanya mabadiliko kwa kumtoa Nico Wadada na kuingia Obrey Chirwa na pia alitoka Chilunda na nafasi yake ilichukuliwa na Idd Kipagwile.
Kwa upande wa Azam, walikuwa wakiongozwa na Yakubu na  Masai ambao walikuwa wanacheza kwa kuelewana, lakini spidi ya mashambulizi ya Simba yalikuwa yakiwachanganya.

SHIBOUB, SURE BOY HABARI NYINGINE
Katika mchezo huo pale katika eneo la kati lilikuwa kama linawaka moto kutokana na namna ambavyo viungo wa timu zote walikuwa wakicheza.
Kwa upande wa Azam, viungo Sure Boy na Domayo waliligeuza dimba la kati kuwa lao, hali iliyowafanya viungo wa Simba Jonas Mkude na Shiboub kutumia nguvu na akili katika kuwadhhibiti.
Sure Boy alikuwa hagandi na mpira mguuni badala yake alikuwa akipata mpira ananyanyua macho haraka na kupiga pasi kwa washambuliaji ambao walikuwa wanatumia vizuri nafasi na muda mwingine wanakosea.
Kwa upande wa viungo Simba, Hassan Dilunga na Shiboub walikuwa wataalamu katika kukaba na kupiga pasi za mwisho.
Shiboub na Dilunga walikuwa nyota katika eneo la kiungo, huku Shiboub akitupia mabao mawili ya kichwa akichagiza ushindi katika klabu ya Simba, lakini uwezo wake wa kucheza pasi za haraka fupifupi na ndefu ameweza kunogesha eneo la katikati Simba.

TSHABALALA VS WADADA
Upande wa kulia kwa Azam alikuwa anacheza beki wa kimataifa kutoka Uganda, Nicco Wadada huku upande wa kushoto Simba akicheza Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.
Wawili hawa walikuwa wanatumika katika kupeleka mashambulizi kwa timu zao, lakini kilichotokea iligeuka bato kali kwa wawili hawa.
Tshabalala alikuwa mwepesi katika kupandisha mipira mbele na alitisha katika kusaidia mashambulizi huku mpira wake wa ‘frii-kiki’ ukizaa bao lililofungwa na Shiboub. Lakini Azam waliufahamu udhaifu wake wa kuchelewa kurudi anapopanda na mipira mingi mirefu ilipelekwa upande wake. Na hata goli la pili la Azam, Obbrey Chirwa alitumia udhaifu wa Tshabalala katika ulinzi, akampita kirahisi mbele yake na kupiga krosi iliyozaa bao la Domayo.
Hali hiyo iliwafanya Simba wamtumie Shomari Kapombe ambaye naye alikuwa mwepesi katika kupandisha mashambulizi, lakini alipoingia Idd Kipagwile alimtuliza.

KAGERE ATULIZWA
Inawezekana katika mchezo huu, Kocha Etienne Ndayiragije alikuwa amewapa kazi maalum wachezaji wake kuhakikisha wanamkaba vilivyo washambuliaji wa Simba, Meddie Kagere na John Bocco.
Kagere ndiye straika hatari wa Simba, lakini katika mchezo huo alidhibitiwa na kushindwa kufanya lolote lile, huku Bocco aliumia mapema kipindi cha kwanza na kutolewa.
Wakati huo huo kwa upande wa Azam, Chilunda aliyerejea kutoka Hispania alipokuwa akicheza kwa mkopo, alionekana kuongezeka udambwi dambwi katika miguu yake kiasi cha kuwasumbua Wawa na Nyoni katika umiliki wa mpira.

SIMBA WALISTAHILI
Licha ya soka la ushindani na mabao matamu yaliyofungwa, lakini kwa hakika Simba walistahili ushindi kwenye mchezo huo kwa namna walivyokuwa wakitengeneza nafasi, licha ya kukosa mabao mengi yangewafanya watoke na kapu Taifa.
Azam ambayo ilichangamka zaidi dakika 20 za mwisho hasa alipoingia Chirwa na Kipagwile, na hakika Ndayiragije atajilaumu kwanini hakumuanzisha mapema Chirwa.

Advertisement