Kipa Nahimana afichua kilichomrejesha kikosini KMC

Muktasari:

Katika mashindano hayo, Nahimana ndiye aliyekuwa kipa tegemeo katika kikosi cha Burundi na aliweza kuonyesha kiwango kizuri kiasi cha kuwafanya mabosi wa KMC kusajili kipa mwingine (Kalambo) kabla ya kuzinguana baadaye.

KIPA wa KMC, Jonathan Nahimana amewashtua baadhi ya mashabiki kutokana na kiwango alichokionyesha kwenye Michuano ya Afcon 2019 akiwa na kikosi cha Burundi, huku ikielezwa asingerejea nchini lakini ghafla jamaa kaamua kurudi tena Tanzania.
Katika mashindano hayo, Nahimana ndiye aliyekuwa kipa tegemeo katika kikosi cha Burundi na aliweza kuonyesha kiwango kizuri kiasi cha kuwafanya mabosi wa KMC kusajili kipa mwingine (Kalambo) kabla ya kuzinguana baadaye.
Mwanaspoti lilizungumza na Nahimana kutaka kufahamu sababu kubwa ya yeye kurejea tena Bongo huku wengi wakiamini alishapata dili lingine baadaya kuchelewa kusaini tena KMC.
Nahimana alisema alikuwa amepata timu lakini wakala wake alikuwa anataka pesa nyingi hali ambayo ilimpotezea dili hizo.
“Sikuwa na malengo ya kubaki tena Afrika Mashariki, lakini wakala ndio amesababisha yote haya baada ya kutaka pesa nyingi, lakini sijakata tamaa bado,” alisema.
Akizungumzia kurejea tena KMC, alisema ni kutokana na namna ambavyo ameishi vizuri na timu hiyo katika msimu uliopita.
“Nikiwa hapa sikuwahi kudai kitu chochote kile yaani, nimeishi vizuri sana na ndio maana nikaona nirejee hapa niwe nacheza wakati nikiwa nasubiri mambo yangu mengine yakae sawa,” alisema.
Nahimana alisema timu ambazo alikuwa anatajiwa na wakala wake kumuhitaji ni Nkana (Zambia), Gor Mahia (Kenya), Petro Atheltico (Angola), Horoya, As Kigali (Rwanda) na nyingine za Msumbiji lakini lolote linaweza kutokea hata katika dirisha dogo.