Soko linasema ukitaka saini zao vunja benki

Sunday August 18 2019

 

London, England. RAHEEM Sterling amewekwa namba tatu katika orodha ya wachezaji wenye thamani kubwa zaidi duniani kwa sasa, huku Mwingereza mwenzake Jadon Sancho akiwa nafasi moja tu nyuma tu ya Lionel Messi.
Orodha ya wanasoka 100, iliyoandaaliwa na kampuni CIES Football Observatory, imetumia mambo kadhaa kupanga thamani za wachezaji hao, ikiwamo umri, mikataba, nafasi za uwanjani, dakika walizocheza, mabao na thamani zao kwenye vikosi vya timu za taifa na mafanikio.
Fowadi wa mabingwa wa Ligi Kuu England, Sterling amepangwa kuwa na thamani ya Pauni 190 milioni, akiwa nyuma kidogo tu ya staa wa Liverpool, Mohamed Salah aliyetajwa kuwa na thamani ya Pauni 200 milioni.
Lakini, mastaa wote hao wamezidiwa na staa wa PSG, Kylian Mbappe, ambaye ndiye mwenye thamani kubwa zaidi, Pauni 230 milioni.
Mbappe alikuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Ufaransa kilichobeba ubingwa wa Kombe la Dunia huko Russia mwaka jana. Supastaa wa Barcelona, Messi, anayehesabika kuwa mwanasoka bora zaidi wa nyakati zote, ameorodheshwa kwenye nafasi ya nne, akipewa thamani ya Pauni 153 milioni.
Hii hapa ndio orodha ya wanasoka 10 wenye thamani kubwa zaidi duniani kwa sasa, kwamba ukiuziwa chini ya hapo, basi umebahatika.
Kwenye orodha hii mastaa kama Paul Pogba, Neymar, Philippe Coutinho, Cristiano Ronaldo, Pierre-Emerick Aubameyang, Eden Hazard wameshindwa kuingia kwenye 10 bora kwa sababu mbalimbali na hivyo kuwafanya mastaa wengine kutamba.
Harry Maguire, Virgil van Dijk, Joao Felix walionaswa kwa pesa nyingi kwa kipindi cha karibuni, wameshindwa kupenya pia katika orodha hiyo ya wakali 10 wa mwanzo wenye thamani kubwa sokoni kwa mujibu wa kampuni hiyo ya CIES Football Observatory. Hii ndio orodha kamili.

Leroy Sane – Man City, Pauni 125 milioni
Staa wa Kijerumani, Leroy Sane kwa sasa hataonekana uwanjani kwa muda mrefu kutokana na kuwa majeruhi, ambapo aliumia kwenye mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Liverpool wiki mbili zilizopita. Staa huyo, ambaye kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi alikuwa anasakwa na Bayern Munich, lakini klabu yake ya Manchester City iliwekwa ngumu kumpiga bei, wakitaka pesa ndefu. Kwa mujibu wa kampuni hiyo, Sane amethaminishwa kuwa na thamani ya Pauni 125 milioni, akikamata namba 10 katika orodha ya wenye thamani kubwa.

Antoine Griezmann – Barcelona, Pauni 131 milioni
Staa fowadi, Antoine Griezmann, hivi karibuni alihama kutoka Atletico Madrid kwenda Barcelona kwa dili la pesa ndefu. Mfaransa huyo, alinyakuliwa kwa Pauni 105 milioni kama ilivyokuwa imeelezwa kwenye mkataba wake, lakini thamani yake sokoni imetajwa kwa sasa kuwa mshambuliaji ukimtaka basi unapaswa kulipa Pauni 131 milioni. Griezmann ameanza vibaya maisha yake huko Nou Camp baada ya kukumbana na kipigo katika mchezo wa kwanza wa La Liga walipochapwa 1-0 na Athletic Bilbao juzi Ijumaa.

Roberto Firmino – Liverpool, Pauni 132 milioni
Unaambiwa hivi, Mbrazili Roberto Firmino ndio injinia wa mipango yote kwenye fowadi ya Liverpool na kwamba asipokuwapo basi mambo mengi yanakwama. Staa huyo amekuwa muhimu kwelikweli kwenye kikosi hicho na Jumatano iliyopita alionyesha hilo kwenye mechi ya Uefa Super Cup wakati alipotoka benchi na kuja kuleta tofauti uwanjani kwenye ushindi wa penalti dhidi ya Chelsea. Ubora wake wa uwanjani umemfanya Firmino kuwa na thamani kubwa na kwamba ukimtaka kwa sasa basi bei yake halali sokoni ni Pauni 132 milioni.

Harry Kane – Tottenham,
Pauni 143 milioni
Straika wa Tottenham Hotspur na timu ya taifa ya England, Harry Kane ni moja ya wanasoka mahiri uwanjani na hakika unapotaka huduma za wachezaji kama hao, basi ni lazima uvunje benki. Kwa muda mrefu, fowadi huyo amekuwa akielezwa kuwa na thamani ya Pauni 200 milioni, lakini taarifa za sasa, zimefichua kwamba Kane ukimtaka bei yake halisi ni Pauni 143 milioni kwa mujibu wa soka. Kane alikosa sehemu kubwa ya msimu uliopita kutokana na kuwa majeruhi na pengine jambo hilo limeshangia kushusha kidogo thamani yake.

Sadio Mane – Liverpool, Pauni 144 milioni
Kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane aliwahi kuripotiwa kwamba amekuwa akiifukuzia huduma ya mshambuliaji wa Liverpool, Msenegali, Sadio Mane. Kuipata au kuikosa huduma ya mshambuliaji kutokana na Liverpool wenyewe kama watakubali kumuuza au kama Los Blancos watakuwa na ofa tamu mezani. Wataalamu wa masuala ya soko na thamani za wachezaji, wamemworodhesha Mane kwenye namba sita kwa wanasoka wenye thamani kubwa duniani, kwamba ukihitaji huduma yake basi ni halali kulipa Pauni 144 milioni.

Jadon Sancho – Dortmund, Pauni 145 milioni
Kinda Mwingereza, Jadon Sancho anaonekana kulishika soka la dunia kwa sasa kutokana na kile anachokifanya huko kwenye kikosi cha Borussia Dortmund. Staa huyo alikuwa moto msimu uliopita akifunga na kuasisti jambo lililowafanya vigogo kibao kufikiria mpango wa kunasa huduma yake. Taarifa za hivi karibuni zinadai kwamba Sancho atakuwa tayari kuihama Dortmund mwakani, lakini kwa timu itakayohitaji saini yake basi itabidi ijipange, maana hawezi kupatikana kwa bei ya chini. Thamani yake ni Pauni 145 milioni.

Lionel Messi – Barcelona, Pauni 153 milioni
Supastaa wa Kiargentina, Lionel Messi kwa sasa ameshavuka umri wa miaka 30, kipindi ambacho kwa wanasoka wengi wanaanza kuonyesha uchovu mkubwa ndani ya uwanja. Lakini, Messi kwenye umri wa miaka 32 haonekani kuchoka, akiwa bado kwenye kiwango bora licha ya kwamba si kama ilivyokuwa miaka kadha iliyopita. Staa huyo siku za karibuni amekuwa akisumbuliwa na majeruhi mara kwa mara, jambo ambalo limemfanya thamani yake kushuka sana, akitajwa kuwa na thamani ya Pauni 153 milioni huko sokoni.

Raheem Sterling – Man City, Pauni 190 milioni
Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola amesema kwamba ana uhakika mkubwa mshambuliaji wake, Raheem Sterling atafunga mara nyingi zaidi msimu huu. Suala la kufunga kwa siku za karibuni halijawahi kuwa gumu kwa Mwingereza huyo na hivyo kiwango chake kumfanya kuwa na thamani kubwa huko sokoni. Man City walimnasa fowadi huyo kwa bei ya kawaida tu kutoka Liverpool miaka kadhaa iliyopita, lakini sasa ukimtaka staa huyo ujipange, maana thamani yake huko sokoni imekuwa kubwa kwelikweli. Sterling ukimtaka Pauni 190 milioni.l

Mohamed Salah – Liverpool, Pauni 200 milioni
Staa Mohamed Salah ni moja ya washambuliaji matata kabisa kwenye soka la ulimwengu kwa sasa. Fowadi huyo wa kimataifa wa Misri amekuwa mchezaji tishio tangu alipotua Liverpool, akibeba Kiatu cha Dhahabu kwenye misimu yote miwili aliyotamba na timu hiyo katika Ligi Kuu England. Uhodari wake wa ndani ya uwanja, umempandisha thamani zaidi Mo Salah, ambaye Liverpool wao walimsajili kwa pesa ndogo sana kutoka AS Roma. Kwa sasa ukimtaka Mo Salah, basi usiwe na mkwanja usifikia Pauni 200 milioni, ndio thamani yake sokoni.

Kylian Mbappe – PSG, Pauni 203 milioni
Utashangaa kwenye orodha hii hakuna jina la Neymar, mwanasoka ghali zaidi duniani kwa sasa, aliyenaswa kwa Pauni 198 milioni miaka miwili iliyopita. Lakini, kwa sasa hata kwenye orodha ya wakali wenye thamani kubwa Neymar ameachwa mbali sana, majeruhi yakimtibulia. Jambo hilo linamfanya staa mwenzake huko PSG, Kylian Mbappe kutamba, akiwa na thamani ya Pauni 203 milioni huko sokoni. Kutokana na hilo, ni halali kumsajili Mbappe kwa Pauni 200 milioni kwa sasa ndio thamani yake kwa mujibu wa watalaamu wa thamani za wachezaji.

Advertisement