Mnahesabu lakini... Arsenal yaichapa mtu pointi sita kibindoni

Muktasari:

Ligi hiyo itaendelea tena leo Jumapili kwa mechi mbili, Sheffield United wakikipiga na Crystal Palace kabla ya Chelsea kushuka Stamford Bridge kusaka ushindi wao wa kwanza kwenye ligi kwa kumenyana na Leicester City.

London, England. ARSENAL inapiga mdogo mdogo tu kwenye Ligi Kuu England baada ya kukusanya pointi sita kwenye mechi mbili na kujitanua kwa dakika kadhaa kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.
Jana Jumamosi, wakiwa uwanjani kwao Emirates, mabao mawili kutoka kwa mastraika wao matata kabisa, Alexandre Lacazette na Pierre-Emerick Aubameyang yalitosha kuwapa ushindi wa 2-1 dhidi ya Burnley.
Ushindi huo umewafanya Arsenal kufikisha pointi sita, huku Burnley wakijaribu kuwatisha kidogo baada ya kufunga bao la kusawazisha katika kupitia kwa Ashley Barnes. Arsenal ilitangulia kufunga kwa bao la Lacazette, Burnley wakachomoa, kabla ya Aubameyang kupiga la ushindi, huku staa wake mpya Unai Emery, aliyemnasa kwa mkopo kutoka Real Madrid, Dani Ceballos akihusika kwenye mabao yote mawili, akitoa asisti mbili.
Katika mchezo huo, Emery alianza na wachezaji wapya wawili, Ceballos na beki wa kati David Luiz, huku mchezaji wake ghali, Nicolas Pepe aliingia kwenye kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Reiss Nelson. Arsenal wamejiweka kwenye nafasi nzuri wakifukuzia mipango yao ya kumaliza msimu huu ndani ya Top Four kwenye Ligi Kuu England.
Ligi hiyo itaendelea tena leo Jumapili kwa mechi mbili, Sheffield United wakikipiga na Crystal Palace kabla ya Chelsea kushuka Stamford Bridge kusaka ushindi wao wa kwanza kwenye ligi kwa kumenyana na Leicester City. Jumatatu usiku kutakuwa na mechi moja, ambapo Manchester United watakuwa ugenini kwa Wolves huko Molineux.