Madrid waibuka kivingine kumnasa supastaa Neymar

Madrid, Hispania. REAL Madrid wameamua kuja kivingine katika mpango wao wa kumsajili supastaa wa Kibrazili, Neymar wakiwaambia Paris Saint-Germain kwamba watawapa Isco, Raphael Varane na Marcelo kwenye dili hilo.

Kocha Zinedine Zidane ameshajiandaa kuachana na baadhi ya mastaa wake ili tu amkamate staa huyo wa Kibrazili anayetaka kuachana na klabu yake ya sasa ya PSG baada ya usajili wa pesa nyingi miaka miwili iliyopita.

Los Blancos wamepanga kumlipa Neymar mshahara wa Pauni 700,000 kwa wiki ili kunasa saini yake, lakini sasa wapo kwenye upinzani mkali na mahasimu wao Barcelona katika vita ya kuwania huduma ya mshambuliaji huyo.

Jambo hilo linadaiwa kwamba ni habari njema kwa Manchester United, kwa sababu wanaamini kumfukuzia Neymar wakimnasa wataachana na mpango wao wa kumsajili kiungo wao nyota, Paul Pogba.

Pogba, alifichua kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi huko Ulaya kwamba anataka kuachana na Man United, lakini Real Madrid wao walianza na usajili wa Eden Hazard, waliyemng'oa Stamford Bridge kwa ada ya Pauni 150 milioni. Sambamba na hilo, Madrid waliwasajili nyota wengine pia kama Luka Jovic, Eder Militao, Ferland Mendy na Rodrygo.

Kocha, Zidane anataka kuboresha kikosi chake kuwa bora zaidi kabla ya msimu mpya wa La Liga kuanza. Lakini, Barcelona nao wanataka huduma ya Neymar na wapo tayari kuwatoa wachezaji Philippe Coutinho na Ousmane Dembele waende PSG.

Mapema kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi, Neymar alisema kwamba anahitaji kurudi nyumbani ambako ni Barcelona. Neymar amewekewa kipengele cha kuuzwa Pauni 198 milioni kwenye mkataba wake, hiyo ina maana itakuwa kiwango kilekile ambacho walimnunua kutoka Barcelona miaka miwili iliyopita. PSG wameacha kuuuza jezi za Neymar wakijiandaa kuachaa na mchezaji huyo.