Temeke yarudisha utemi Ndondo Cup

Baada ya unyonge wa miaka miwili mfululizo, Wilaya ya Temeke imerudisha utemi wake kwenye mashindano ya Ndondo Cup mwaka huu baada ya timu ya UV Temeke kuibuka bingwa mbele ya Uruguay.

Ushindi wa mikwaju ya penati 5-3 ulitosha kwa timu hiyo ya Temeke kuibuka bingwa wa mashindano hayo baada ya mechi hiyo kumalizika kwa sare ya bao 1-1 katika dakika 90 za mchezo.

Mechi hiyo ililazimika kuamriwa kwa mikwaju ya penati baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

UV Temeke walilazimika kutoka nyuma na kupata ushindi huo baada ya kutanguliwa kwa bao la mapema kipindi cha kwanza la Uruguay lililofungwa na nyota wa zamani wa African Sports, Chinu Kofia Mbaya.

Lakini wakati kila mmoja akiamini Uruguay wataibuka washindi wa mechi hiyo, Hamis Ngoengo aliwainua vitini umati wa mashabiki wa UV Temeke baada ya kuipachikia bao la kusawazisha katika dakika za lala salama.

Matokeo hayo yaliipeleka mechi hiyo kwenye mikwaju ya penati ndipo UV Temeke walipoitoa kimasomaso wilaya yao kwa kupata penati zote tano huku wapinzani wao wakikosa moja.

Penati hizo tano za UV Temeke zilifungwa Dickson Mhilu, Yahaya Mbegu, Samuel Jackson, Salvatory Ntebe na Godfrey Wambura

Upande wa Uruguay waliofunga ni Sabri Rashid, Moses Kitandu, Muhsin Nganda huku Idrisa Chaulembo akikosa

UV Temeke inakuwa ni timu ya pili kutoka Temeke kutwaa ubingwa wa mashindano hayo baada ya Temeke Market iliyofanya hivyo mwaka 2016.

Timu nyingine ambazo zimewahi kutwaa ubingwa wa mashindano hayo ni Abajalo, Faru Jeuri, Manzese United na Misosi FC.

Ni mechi ambayo ilijaa vituko vingi vya nje ya uwanja kuanzia kabla na hata wakati timu zilipowasili kabla ya kuanza kwa mechi.

Uruguay ndio walikuwa wa kwanza kuwasili uwanja hapo mnamo saa 9.15 mchana ingawa hawakuingia katika eneo la kuchezea huku wakiamua kufanyia mazoezi ya kupasha misuli nje ya uwanja.

Mara baada ya timu hiyo kuwasili, kocha wa Uruguay, Adam Seseme alienda ndani ya eneo la kuchezea na kukatisha katikati ya kiwanja kisha kwenda kukaa kwenye benchi la timu hiyo.

Baadaye mnamo saa 9.30 UV Temeke nao waliingia ndani ya eneo la uwanja huo na kuingia moja kwa moja katika sehemu ya kuchezea na kuanza kupasha misuli.

Katika hali ya kushangaza, UV Temeke waliingia wakiwa wamegeuza jezi zao na walipoanza kupasha, ghafla walitoka nje na kubadilisha jezi zao na kuzivaa kama ilivyo kawaida tukio ambalo lilitokea wakati Uruguay walipoingia uwanjani.

Wakati huo UV Temeke wanapasha misuli, mashabiki watatu wanaosadikiwa ni wa Uruguay, walikuwa wakizunguka uwanja huo huku wakimwaga chumvi.

Mechi hiyo ilihudhuriwa na viongozi kadhaa wa serikali pamoja na wadau wakubwa wa mpira wa miguu nchini waliojitokeza kwa wingi wakiongozwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza.

Pia alikuwepo Naibu Waziri wa Maji, Juma Aweso, Makamu wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Athuman Nyamlani.

Ukiondoa hao,pia kulikuwa na katibu mkuu wa TFF, Wilfred Kidao, Meya wa Ilala, Omary Kumbilamoto na mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Dar es Salaam (DRFA), Almas Kasongo.

Katika hotuba yake kabla ya kuanza kwa mechi hiyo ya fainali,Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza alizotaka timu na wachezaji kuyatumia vyema mashindano hayo.

Pamoja na malengo ya kitimu, mashindano haya lengo lake kuu ni kuibua vipaji vya vijana. Kama mnavyofahamu kwamba kuna vijana ambao sasa wanachezea timu mbalimbali za Ligi Kuu mfano Yanga, Lipuli na nyinginezo.

Hivyo mcheze kwa juhudi ili muyatumie mashindano haya yawe fursa kwenu kuonyesha vipaji vyenu," alisema Waziri Shonza.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso aliishauri wizara ya michezo kuwapa sapoti waandaaji wa mashindano hayo.

"Vijana hawa wanatekeleza agizo la mheshimiwa Rais la kufanya kazi, hivyo mheshimiwa naibu waziri naomba muwatazame ndugu zetu wa Clouds kwa kuandaa mashindano haya ambayo yamekuwa fursa ya ajira kwa vijana," alisema Waziri Aweso.