Jicho la Mwewe: Umefika muda wa Juuko na Simba kuachana rasmi

Muktasari:

Sijui kimsingi sana kilichoendelea baina yao lakini vigogo wengi wa Simba wanadai Juuko ni tatizo. Ushahidi wa mazingira unaonyesha inawezekana. Mbona kinachomtokea Juuko hakikumtokea Paschal Wawa? Mbona hakikumtokea James Kotei wala Nicolas Gyan? Juuko anasema anaidai Simba mishahara ya miezi mitatu.

MASHABIKI wa Simba, na klabu nyingine za Tanzania, huwa tunakodolea macho televisheni zetu pindi mechi za timu ya Taifa ya Uganda zinapoonyeshwa. Mara zote huwa tunamuona Juuko Murshid akicheza. Huwa anapambana kwelikweli. Ni beki tegemeo kule. Huwa tunabaki midomo wazi. Klabu yake ni Simba, lakini Simba na Juuko hawana urafiki mzuri kuliko Juuko na The Cranes. Sio mchezaji tegemeo wa kiasi hicho. Ni kitu cha kawaida kumuona Juuko akiwa benchi. Kitu cha kawaida kabisa. Ni kawaida kusikia Juuko hayupo katika kambi ya Simba.
Waganda wametuzidi mpira. Karibu wachezaji wao wote wa kikosi cha kwanza cha timu ya Taifa hawawezi kukosa namba katika klabu zetu tatu hapa nchini. Iwe Juuko mwenyewe, Godfrey Walusimbi, iwe Hassan Waswa, Kipa Denis Onyango, Emmanuel Okwi na wengineo. Kwanini Juuko awe na nafasi ya kusuasua Simba?
Uchunguzi wa haraka ukanionyesha Juuko mwenyewe ni tatizo. Ni aina ya wachezaji fulani wa kigeni ambao mfumo wetu wa soka uliwalea vibaya walipofika nchini. Wakajisahau kwamba wao ni wachezaji wa kulipwa na kazi yao ni kucheza soka.
Sijui kimsingi sana kilichoendelea baina yao lakini vigogo wengi wa Simba wanadai Juuko ni tatizo. Ushahidi wa mazingira unaonyesha inawezekana. Mbona kinachomtokea Juuko hakikumtokea Paschal Wawa? Mbona hakikumtokea James Kotei wala Nicolas Gyan? Juuko anasema anaidai Simba mishahara ya miezi mitatu. Siamini kama Simba ya sasa inaweza kumnyima mchezaji mishahara ya miezi mitatu. Siamini. Lazima kuna jambo. Simba haikabiliwi na tatizo lolote kubwa kipesa. Inawalipa wachezaji wake vema. Hatujasikia malalamiko kutoka kwa wachezaji wanaolipwa mishahara mikubwa kama Meddie Kagere, vipi kuhusu Juuko?
Zaidi ya yote, hakuna mchezaji wa Simba anayeidai klabu hiyo miezi mitatu. Kwanini yeye peke yake? Ina maana mabosi wa Simba waliamua kuwalipa wachezaji wengine wote kisha ikakataa kumlipa Juuko bila ya sababu?
Juuko angeeleza kwanza sababu ambazo zimewafanya viongozi wa Simba kumnyima mshahara wa miezi mitatu na sio kuiripoti habari kama ilivyo. Hakuna viongozi wendawazimu katika Simba ambao wanaweza kutomlipa Juuko mshahara wa miezi mitatu.
Juuko anadai viongozi wa Simba hawamthamini. Hili nalo siliamini sana. Viongozi wetu wanababaikia sana wachezaji wenye uwezo mkubwa. Wawe wa kigeni au wa ndani. Kwanini amedumu klabuni hapo kwa muda mrefu? Nadhani ni mchezaji wa kigeni aliyedumu zaidi klabuni.
Kinachofurahisha zaidi ni kwamba wachezaji wasiothaminika ndani ya klabu hizi huwa wana maisha mafupi tu. Unaweza kukatwa siku moja kabla ya kufungwa kwa dirisha la uhamisho. Unaweza kutolewa kwa mkopo siku chache baada ya kupewa mkataba.
Sina nia ya kuwatetea Simba katika hili lakini ukichungulia kwa nje ni wazi utagundua Juuko ni zao la wale wachezaji wa kigeni walioingia klabuni hapo mitaa ya kati na kulelewa kijamaa. wachezaji ambao walikuwa wanachelewa kurudi kutoka likizo au katika kambi ya timu zao za taifa.
Kitu cha msingi kwa sasa ni kwa Simba kuachana na Juuko. Hawawezi kuishi kama wanavyoishi. Ni sawa kuwa na mpenzi ambaye kila siku mnagombana. Haiwezekani mchezaji wa kudumu katika kikosi cha Cranes akawa sio mchezaji tegemeo katika kikosi cha Simba, Yanga au Azam FC. Kwa muundo wa mpira wetu, haiwezekani. Mchezaji wa namna hiyo atakuwa na shida.
Juuko anahitaji changamoto mpya kwingineko. Beki wa kudumu wa The Cranes lazima awe na uhakika wa namba klabuni, lakini pia lazima awe na furaha kwa ajili ya kuendelea kuwa na namba ya kudumu kikosini.
 Simba nayo inahitaji kuwa na wachezaji walio kamili kimwili na kiakili. Wanakoelekea kwa sasa hawapaswi kuwa na muda wa kubembelezana na wachezaji wao.
Hili la Juuko lazima waone linafika tamati. Maamuzi ya pande zote mbili ni ya kiweledi katika soka (Professionalism). Klabu haipaswi kuwa na mchezaji ambaye hana furaha, na mchezaji hapaswi kukaa katika klabu ambayo hana furaha nayo. Kwanini kung’ang ’aniana? Ni muda mwafaka kwao kuachana. Hakuna ambaye atashangaa. Kinachoshangaza ni kwa Juuko kuendelea kuwa mchezaji tegemeo The Cranes huku akiwa hana uhakika wa maisha yake ndani ya Simba. Hivi tunavyozungumza ni mchezaji wa Simba lakini hayupo katika kambi Afrika Kusini.
Nasikia mkataba wake unamalizika Desemba mwaka huu. Ningekuwa kiongozi wa Simba ningekutana naye na kuachana naye kwa makubaliano yenye maslahi kwa pande zote (Mutual agreement).
Kama Simba wanataka labda kumuuza katika dirisha hili bado itashangaza kidogo kwa sababu amebakiza miezi michache ambayo haiwezi kumfanya awe mchezaji mwenye thamani. Nadhani thamani yake haiwezi kuzidi kero ambazo inazipata kutoka kwa mchezaji mwenyewe.