Patel:Nilitumia dakika 10 kufanya uamuzi Afcon U17

Thursday May 2 2019

Mwanaspoti, Michezo, Michezo blog, Mwanasport, Patel, Nilitumia, dakika 10 ,kufanya uamuzi, Afcon U17, MICHEZO

 

By Imani Makongoro

Dar es Salaam. Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Kampuni za Motisun Group, Subash Patel amesema alitumia dakika 10 kufanya uamuzi wa kusaidia kufanikisha mashindano ya Afrika kwa vijana (AFCON U17) yaliyofanyika nchini.
Patel ametamka hayo leo baada ya kutembelewa na Kamati ya Maandalizi ya Mashindano hayo nchini ofisi kwake kwa lengo la kutoa shukrani kwa kampuni hiyo kwa mchango wake.
"Nilipofuatwa ili kufanikisha Afcon, sikujiuliza mara mbili, tulitumia dakika 10 tu katika mazungumzo yetu na tukaamua kuwa sehemu ya mashindano," alisema Patel.
Kwa mujibu wa Aliyekuwa mtendaji mkuu wa mashindano hayo upande wa Tanzania, Leslie Liunda, Patel alisaidia malazi na vinywaji kwa kipindi chote cha mashindano.
"Alitoa maji ambayo yalitumika kipindi chote cha mashindano, kwenye mechi, mazoezi na kwa viongozi, na juisi.
"Viongozi wa juu wa CAF kuanzia rais na viongozi wengine 17 walikaa Sea Criff Hoteli kwa gharama zake.
"Hakuishia hapo, wageni ambao walialikwa na CAF na TFF walikaa Whitesands kwa gharama zake, kuanzia malazi na chakula," alisema.
Alisema mchango huo ambao umetolewa na Patel ni wa kipekee ndiyo sababu wamelazimika kurudisha shukrani zao kwake kwa kuwa sehemu ya kufanikisha mashindano," alisema.
Patel alisema amefurahi kuwa sehemu ya mashindano ya Afcon kwani ni kitu kikubwa kufanyika nchini.
"Kutoa ni moyo, hivyo niwashauri tu Watanzania wenzangu wenye moyo wa kuchangia wawe wanajitolea katika matukio kama haya, kwani uenyeji wetu wa Afcon ni mwanzo mzuri kuelekea kuandaa mashindano makubwa," alisema Patel.

Advertisement