Hebu msikieni Sarri anachosema Chelsea

Monday March 18 2019

 

London, England. Huyu Maurizio Sarri si bure amerogwa. Hivi umesikia alichokisema baada ya kikosi chake cha Chelsea kuchapwa na Everton kwenye Ligi Kuu England Jumapili huko Goodison Park? Eti hata hajui kwanini wamepoteza mechi hiyo.
Kocha huyo Mtaliano alisema hafahamu kilichotokea hadi wakapoteza mechi hiyo wakati kikosi chake kilimiliki mpira kuanzia mwanzo hadi mwisho. Lakini, mwisho wa mchezo, The Blues walichapwa 2-0 na hivyo kumaliza kabisa matumaini ya kukamatia nafasi kwenye Top Four katika Ligi Kuu England.
Bosi huyo aliyekalia kuti kavu huko Stamford Bridge, alisema: “Sijui nini kimetokea. Wachezaji nao hawajui nini kimetokea, kwa kweli siwezi kuelezea kitu. Mpira tumecheza, ukiniuliza nitakwambia hivyo.
"Tulikuwa na kipindi cha kwanza bora kabisa na nadhani tungeweza kufunga mabao manne au matano, ghafla tu tukaacha kucheza. Ni kitu kinachoshangaza sana."
"Tukaacha kukaba na wao wakashambulia kwa kushtukiza. Ghafla tukawa timu tofauti, kwa kweli mi sifahamu. Vitu vya ajabu sana, sielewi kabisa."
Kwa kipigo hicho cha Jumapili kimewafanya Chelsea sasa kupoteza mechi saba kwenye Ligi Kuu England huku kikosi hicho kikishika nafasi ya sita kwenye msimamo pointi tatu nyuma ya Arsenal walipo kwenye nafasi ya nne inayotoa tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Advertisement