Klopp aringia ubora wa kikosi chake

Saturday January 25 2020

 Klopp aringia ubora wa kikosi chake-Jurgen Klopp -Ligi Kuu England -

 

LIVERPOOL, ENGLAND .KIPATO huleta majivuno wanasema. Eti Jurgen Klopp alitaka kutapika baada ya kuwambiwa kwamba chama lake la Liverpool linaweza kupoteza mechi sita na bado itabeba taji la Ligi Kuu England msimu huu.
Kocha huyo Mjerumani alisema ushindi wa mabao 2-1 iliyopata timu yake dhidi ya Wolves usiku wa juzi Alhamisi, ilikuwa ngumu kwelikweli, lakini ameshukuru timu yake kuweka pengo la pointi 16 kileleni, timu ikishinda mechi 22 kati ya 23 ilizocheza kwenye ligi msimu huu, huku wakiweka rekodi ya kucheza mechi 40 bila ya kupoteza kwenye ligi.
Lakini, Klopp hakuzisikia vizuri baada ya kuambiwa kwamba anaweza kupoteza hadi mechi sita na bado timu yake itabeba taji lake la kwanza la ligi tangu mwaka 1990.
"Hii meseji ya kwamba kupoteza mechi sita inanitia kichefuchefu," alisema.
Wakati hilo likisemwa kuhusu Liverpool ya msimu huu, staa wa miamba hiyo ya Anfield, Sadio Mane amefichua siri kwamba wachezaji wote wa kikosi hicho wamekuwa wakiwahi mazoezi saa moja kabla ya kuanza vipindi vya kufanya mazoezi hayo. Alisema kawaida, wachezaji wamekuwa wakiwahi mapema sana na kuingia kwenye gym na baada ya hapo, ndipo mambo mengine yanaendelea na ratiba za mazoezini kama zilivyo. Staa Mane alipata majeruhi kwenye mchezo huo wa Molineux na kushindwa kumaliza mechi.
"Mashabiki wanaona pale tu wanapokuja uwanjani kwenye mechi za kila wikiendi. Lakini, sisi kama wachezaji tumekuwa tukijianda kuanzia nyumbani na kufanya kazi kubwa mazoezini. Tangu siku ya kwanza niliyokuja hapa, wachezaji wamekuwa wakiongezeka viwango vyao kutokana na nidhamu ya mazoezini, wanawahi asubuhi sana, wanaingia gym kabla ya kuanza rasmi ratiba ya mazoezi ya siku husika," alisema Mane.

Advertisement