He! Baba Diamond, Baby Madaha wapagawa msituni

Saturday July 13 2019

 

By Mwandishi wetu

BABA mzazi wa staa wa Bongo Flava, Diamond Platnumz, Abdul Naseeb ameweka wazi ndoto yake ya kuwa Balozi wa Msitu wa Asili wa Magamba uliopo wilayani Lushoto mkoani Tanga.
Mzee Abdul alipata hamu ya kuutangaza msitu huo na vivutio vyake mwishoni mwa wiki iliyopita, kufuatia ziara waliyofanya waandishi wa habari za burudani pamoja na mzee huyo aliyeongozana na staa mwingine wa filamu na muziki, Baby Madaha.
Katika ziara hiyo ambayo ilichukua siku nzima msituni humo, baba Diamond na Baby Madaha waliyashuhudia mengi ya kuvutia ambapo walitua hadi kwenye bwawa jeusi.
Bwawa hilo ambalo lina maji meusi kimtazamo, limetulia na kutomshwishi mtu kudumbukia kwa lengo la kuogelea zaidi ya mtu kutamani kuendelea kulitazama kwa mbali.
Afisa Utalii na Mafunzo  wa msitu huo wa Magamba, Samiji Mulemba alisema kuwa weusi wa maji ya bwawa hilo unatokana na kuzungukwa na msitu mzito ambao vivuli vyake vinakwenda hadi ndani ya maji.
Hata hivyo, alisema kuwa bado hawajaruhusu watalii na watu wengine kuingia ndani ya bwawa hilo kwa kuwa halijafanyiwa uchunguzi wa kina kujua usalama wake.
Bwawa hilo linadhaniwa kuchimbwa na tajiri aliyefahamika kwa jina la Grewal, ambaye alikuwa akijishughulisha na uvunaji wa mbao za asili kabla ya uhuru wa nchi Tanganyika.
Akizungumza ndani ya msitu huo, Mzee Abdul alisema atamshauri Diamond na timu yake ya Wasafi Classic Baby (WCB) kwenda kutembelea msitu wa Magamba ili kujionea raha za dunia ambazo zinapatikana kwenye maeneo mbalimbali nchini.
"Huu misitu nilikuwa nauona kwenye filamu za kivita za kina Rambo, nikajua ipo nje tu wala sikujua kama nchi yetu ina mambo mazuri kama hayo," alisema.
"Nikipata fursa kamili ya kuwa Balozi wa Magamba, nitahakikisha kunakuwa na ziara ya wasanii kila mwaka msituni hapa," alisema.

Advertisement