Bondia wa Mwakyembe alichapwa ngumi 28 kwa dakika tano

Wednesday June 19 2019

 

Dar es Salaam.Bondia Seleman Bangaiza licha ya Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe kuagiza afungiwe, lakini alichezea kipigo cha nguvu Austarlia.
Bangaiza alipigwa kwa Technical Knock Out (TKO) raundi ya pili ya pambano lililokuwa la raundi 10 dhidi ya Andrew Moloney
Kabla ya kusalimu amri, Video fupi ya pambano hilo inamuonyesha Bangaiza akiwa amesimama kwenye kona yake wakati mpinzani wake,  akipanga ngumi, Bangaiza alinyoosha mkono juu kuonyesha ishara ya kutoendelea na pambano kisha akatema kilinda ulimi (mouth guard).
Baada ya tukio hilo, refarii alionyesha ishara ya kumaliza pambano huku Moloney akimpa tano Mtanzania huyo ambaye alikubali kipigo cha TKO raundi ya pili.
Hata hivyo, video 'full' ya pambano hilo inaonyesha Bangaiza alimpiga mpinzani wake ngumi 13 yeye alipigwa ngumi 28 katika dakika tano walizocheza.
Dakika tatu za raundi ya kwanza, Bangaiza alipigwa ngumi 15 huku yeye akimpiga mpinzani wake ngumi sita usoni, kwenye mbavu na kichwani na raundi ya pili alicheza kwa dakika mbili ambapo alipigwa ngumi 13 na yeye kumpiga Muaustralia ngumi saba.
Baada ya kipigo hicho, kocha aliyeambatana na Bangaiza, Anthony Rutha alisema promota wa Australia amemnyima malipo ya pambano bondia huyo huku Juzi Jumatatu Waziri Mwakyembe akiagiza afungiwe kabla ya Jana Jumanne kamisheni ya ngumi za kulipwa Tanzania (TPBRC) kutangaza kumsimamisha.
Licha ya adhabu hizo, video 'full' ya pambano la Bangaiza na Moloney zinamuonyesha Bangaiza akielemewa na ngumi mfululizo za mpinzani wake, kabla ya kudondoka chini lakini refarii akasema hakudondoka sababu ya ngumi bali aliteleza.
Raundi ya kwanza, mpinzani wake alikuwa akipiga ngumi za kudokoa, huku akipiga nyingine za kwenye mbazi na moja ya kulia 'uppercut' ambayo ilimuingia Bangaiza na kuonyesha ishara ya kuikubali kabla hajasalimu amri raundi ya pili.
Japo kocha aliyeambatana naye Australia, Anthony Rutha alisema hajui sababu za bondia huyo kupigwa, kwani alikuwa fiti na hakuna punch ambayo alipigwa kusema ilimlevya hadi kuacha pambano.
Bondia Kanda Kabongo alisema ameangalia video ya pambano hilo, Bangaiza amepigwa kihalali kwani kuna ngumi alipigwa raundi ya pili ikamlevya.
Akizungumzia pambano hilo, Bangaiza alisema hajaauza kama ambavyo baadhi ya watu wanafikiri, lakini alijikuta imetokea tu akalazimika kuacha pambano.
Advertisement