Bodi ya Ligi waikomalia Yanga

Friday August 23 2019

 

By Charity James

YANGA kesho Jumamosi watakuwa na kibarua ugenini nchini Botswana dhidi ya Township Rollers, lakini huku nyuma Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB), Boniface Wambura amekomaa nao akidai siku tatu walizonazo baada ya mchezo wao huo zinawatosa kuliamsha kwenye Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting.
Uongozi wa Yanga uliomba mechi hiyo iliyopangwa kuchezwa Jumatano ijayo kusogezwa mbele kwani wachezaji watarejea nchini wakiwa wamechoka, lakini Wambura alisema wajipange tu kwa mchezo kama ratiba inavyoonyesha.
Wambura amesema hawapo tayari kubadilisha ratiba ya ligi msimu huu na kusisitiza kuwa itakuwa na utofauti mkubwa na misimu iliyopita kwani msimamo wao utakuwa ni kuhakikisha timu zinafuata ratiba.
"Yanga walituandikia barua kuomba tusogeze mbele mchezo wao, sisi tumewajibu kuwa hatutobadilisha ratiba ya mchezo wowote wa ligi, wao wanasema wanacheza Agosti 24 hvyo wana muda mfupi wa kujiandaa. Lakini sisi ratiba yetu tulishaitoa," amesema Wambura.
Pazia la Ligi linafunguliwa kesho Jumamosi kwa michezo mitano, huku wawakilishi hao wa Tanzania, Yanga pamoja na Simba, KMC na Azam wakipangiwa kuanza kibarua chao kuanzia Jumanne hadi Alhamisi ya wiki ijayo mechi zote zikichezwa jijini Dar es salaam.
Azam wataanza kazi dhidi ya KMC Jumanne kisha Jumatano kuwa zamu ya Yanga na Alhamisi Simba itaumana na JKT Tanzania.

Advertisement