Biashara United waishitaki Alliance TPLB

Friday September 20 2019

 

By SADDAM SADICK, MWANZA

KLABU ya Biashara United imeiandikia barua Bodi ya Ligi Kuu nchini (TPLB) kufuatia vurugu walizofanyiwa na Alliance FC muda mchache kabla ya mechi yao kuanza na kusababisha baadhi ya wachezaji wao kuumizwa na kukosa mpambano huo.
Afisa Habari wa timu hiyo, Shomari Binda amesema kitendo walichofanyiwa na Alliance wakati wakiingia uwanjani si cha kiungwana na kwamba tayari wameandika barua ili hatua zichukuliwe.
"Wakati timu inaingia uwanjani mashabiki wa Alliance walituzuia tusiingie uwanjani wakiwa na viongozi wao na wakati tunajiuliza, wachezaji wetu watatu Ramadhan Chombo, Innocent Edwine na Justine Omary walipigwa hadi kuumizwa na hata Chombo ameshindwa kucheza," amesema Binda.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Mashindano ya Alliance FC, Yusuph Budodi amesema hakuna kiongozi aliyehusika katika vurugu hizo, isipokuwa ni mashabiki wa pande mbili ambao walishindwa kutumia busara.
"Hakuna kiongozi wa Alliance aliyehusika na hili naomba TFF  (Shirikisho la Soka nchini) lifuatilie kwa umakini isije kuonekana ni upande mmoja hata sisi tunalaani vitendo hivi" amesema Budodi.
Katika hatua nyingine Budodi ameeleza kuwa hata vurugu walizofanyiwa Kagera Sugar kukumbana na vurugu wakati wanaingia uwanja wa Nyamagana kufanya mazoezi kuwa hilo halifahamu kwani lilitokea nje ya uwanja.
"Kuhusu tukio la Kagera Sugar tuliachie mamlaka (Polisi) kwani sikuwepo wakati wa vurugu na hilo lilikuwa ni nje ya uwanja, baada ya Kagera Sugar kulazimisha kuingia bila kufuata utaratibu waliopewa na walinzi" amesema Budodi.
Mratibu wa Kagera Sugar, Paul Ngalyoma amesema katika vurugu hizo zimepelekea gari lao kuvunjwa vioo, huku Kocha Mkuu, Mecky Maxime, Msaidizi wake Ally Jangalu na Kocha wa Makipa Mussa Mbaya kujeruhiwa.
"Hiki kitendo si cha kiungwana lakini tunashukuru Polisi wamefika na kuwakamata wahusika na haiwezi kutuharibu kisaikolojia kuelekea mchezo wetu wa kesho dhidi ya Mbao," amesema Ngalyoma

Advertisement