Arsenal, Man U waibeba England

Muktasari:

  • Urejeo wa Ligi ya mabingwa  Ulaya na Europa  kwa msimu  huu, umekuwa na msisimko wa aina yake  kutokana na aina ya matokeo yaliyopatikana  kwenye michezo ya mzunguko  wa kwanza  katika hatua ya makundi ambayo imeanza kutimua vumbi.

LONDON, England. BAADA ya klabu za England kuchemsha vibaya kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, usiku wa jana Wapiga Mitutu wa Arsenal na Man United imefuita makosa kwa kupata ushindi kwenye michezo yao ya Ligi ya Ulaya (UEFA Europe League), huku wababe Wolverhampton Wanderers wakichezea kichapo dhidi ya Braga ya Ureno.
Mashetani Wekundu wakiwa Old Trafford, waliikaribisha FC Astana ya Kazakhstan na kuifunga bao 1-0, lililofungwa na kinda, Mason Greenwood.
Katika mchezo huo, Ole Gunnar Solskjaer alionekana kutoa nafasi kwa makinda ambapo katika eneo la ulinzi walicheza, Diogo Dalot (20) na Axel Tuanzebe (21) huku maeneo mengine wakicheza Tahith  Chong (19), Angel Gomes (19) na mzoefu, Marcus Rashford mwenye miaka 21.
Arsenal ambao walikuwa Ujerumani kucheza na Eintracht Frankfurt, waliibuka na ushindi wa mabao 3-0, yaliyofungwa na Joseph Willock, Bukayo Saka na  Pierre-Emerick Aubameyang.
Kocha wa Arsenal, Unai Emery naye alikifumua kikosi chake cha kwanza anachokitumia  kwenye michezo ya Ligi Kuu England kwa kuwapa nafasi makinda kama vile, Bukayo Saka (18), Emile Smith Rowe (19) na Joseph Willock mwenye miaka 20.
Wawakilishi wengine wa England kwenye Europa Ligi, Wolves walikiona chamoto nyumbani kwa kukubali kipigo cha bao 1-0, walilofungwa na Ricardo Horta wa Braga.
Kipigo cha Wolves ni cha tatu kwa timu za England katika michezo yao ya kwanza katika Europa na Ligi ya Mabingwa, waengine walioanza vibaya ni Chelsea waliopigwa na Valencia na Liverpool ambao walifungwa na Napoli.
Vigogo wa England ambao wameanza vizuri mbali na Manchester United na Arsenal kwenye Europa Ligi, wengine ni Manchester City ambao waliifunga Shakhtar Donetsk ambao 3-0 na walau Tottenham Hotspur ambao walitoka sare ya mabao 2-2 ugenini dhidi ya Olympiacos kwenye Ligi ya Mabingwa.