Zubimendi ni suala la muda tu Arsenal

Muktasari:
- Zubimendi, 26, amekubali dili la Pauni 51 milioni kujiunga na miamba hiyo ya Emirates na sasa yupo kwenye hatua za mwisho kukamilisha uhamisho wake kabla ya kutangazwa rasmi kuwa mchezaji mpya wa Arsenal.
LONDON, ENGLAND: KIUNGO wa Kihispaniola, Martin Zubimendi ameripotiwa kutua London kwenda kukamilisha mpango wake wa kujiunga na Arsenal kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Zubimendi, 26, amekubali dili la Pauni 51 milioni kujiunga na miamba hiyo ya Emirates na sasa yupo kwenye hatua za mwisho kukamilisha uhamisho wake kabla ya kutangazwa rasmi kuwa mchezaji mpya wa Arsenal.
Real Madrid iliingia dakika za mwisho kwenye mpango wa kumsajili staa huyo wa Real Sociedad, lakini tayari Arsenal ilikuwa imeshapiga hatua nzuri katika kunasa huduma ya mtu wao iliyoanza kumfukuzia tangu dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana.
Arsenal imekuwa ikimfukuzia kiungo huyo kwa misimu kadhaa sasa, ambapo Kocha Mikel Arteta amekuwa shabiki mkubwa wa staa huyo wa Hispania, ambaye aliisaidia nchi yake kuichapa England na kushinda ubingwa wa Euro mwaka jana.
Arsenal inapambana kuboresha safu yake ya kiungo baada ya Jorginho kuondoka, huku staa wa Ghana, Thomas Partey naye akidaiwa kuachana na timu hiyo ya Emirates baada ya kushindwa kuafikiana juu ya mkataba mpya baada ya huu wa sasa kufika ukomo Juni 30.
Arsenal ina matumaini Zubimendi ataanzisha zama za usajili wa mastaa kwenye kikosi hicho cha Emirates chini ya mkurugenzi wa michezo mpya, Andrea Berta, ambaye pia atakuwa kwenye kasheshe zito la kusaka straika mpya na winga wa kushoto.
Berta amekuwa akizifanyia sehemu nyingine pia kwenye koikosi ili kutengeneza timu yenya nguvu ya kushindana kwenye Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Bosi huyo kwenye rada yake ya mastraika yupo mkali wa RB Leipzig, Benjamin Sesko na wa Sporting Lisbon, Viktor Gyokeres na mkali wa Aston Villa, Ollie Watkins - ambaye ilianza kumfukuzia tangu kwenye dirisha la Januari.