Xavi Simons katua Spurs
Muktasari:
- Lakini, mkali huyo amegoma kwenda kuvaa uzi wa The Blues huko Stamford Bridge na badala yake amechagua kujiunga na mahasimu wao wa London, Tottenham Hotspur.
LONDON, ENGLAND: HATIMAYE, Xavi Simons amekamilisha uhamisho wake wa kutua kwenye Ligi Kuu England.
Lakini, mkali huyo amegoma kwenda kuvaa uzi wa The Blues huko Stamford Bridge na badala yake amechagua kujiunga na mahasimu wao wa London, Tottenham Hotspur.
Mdachi huyo amekamilisha uhamisho wake wa Pauni 52 milioni huko Spurs, ambako amesaini mkataba wa miaka mitano na kipengele cha kuongeza miwili zaidi.
Kocha mpya wa Spurs, Thomas Frank, amekuwa kwenye msako wa kutafuta Namba 10 mpya kwenye timu yake baada ya James Maddison kuumia kwenye kipindi hiki cha majira ya kiangazi na sasa imempata mchezaji mwenye uwezo wa kucheza nafasi hiyo.
“Nimefurahi sana kwa kumsajili Xavi ni ongezeko bora kwenye kikosi,” alisema Frank.
“Bado kijana, lakini tayari ana uzoefu wa kutosha kutokana na kiwango cha juu kabisa cha soka anachocheza. Xavi ameonyesha uwezo mkubwa wa kufunga mabao na asisti, akiweza kucheza Namba 10 na wingi ya kuchoto. Ni mzuri pia katika kuwasaidia wenzake uwanjani kutokana na uwezo wake wa kupenya ngome za ulinzi za timu pinzani.”
Na baada ya uhamisho huo, staa huyo mpya wa Spurs, ambaye atavaa jezi Namba 7 alisema: “Nimefurahi sana na naona nachelewa kuanza kuichezea timu yangu. Nimekuwa kwenye ndoto ya hili kwa muda mrefu. Ni klabu kubwa na wakati nilipokutana na kocha mkuu, nilijua ni mahali sahihi. Nitaleta burudani kwenye timu na kupambana kwa nidhamu kubwa.”
“Nataka kufanya kila kitu ninachoweza ili kushinda kwa ajili ya timu na mashabiki.”
Spurs imeanza msimu huu kwa ushindi katika mechi mbili za kwanza, huku ikiwa kwenye kipindi kigumu kwa kuwakosa mastaa wake muhimu Maddison na Dejan Kulusevski kabla ya kushindwa kumnasa pia Eberechi Eze, aliyewatosa katika dakika za jiooni na kutimkia kwa mahasimu wao Arsenal na pia iligonga mwamba kwenye msako wao wa kumsajili Morgan Gibbs-White.
Kuhusu Simons kwenye dirisha hili alikuwa kwenye rada za timu kibao ikiwamo Chelsea, ambayo sasa itaongeza nguvu kwenye kumsajili winga wa Manchester United, Alejandro Garnacho.