Wissa njiani Kaondoka Brentford
Muktasari:
- Wissa, 28, amekuwa ahusishwa na mpango wa kuachana na Brentford kwenye dirisha hili la usajili huku klabu hiyo ikigomea ofa ya Pauni 25 milioni kutoka Newcastle United.
LONDON, ENGLAND: STAA wa Brentford, Yoane Wissa ameondoka kwenye kambi ya mazoezi ya timu hiyo ya pre-season wakati huu akiwa hafahamu hatima ya maisha yake ya baadaye.
Wissa, 28, amekuwa ahusishwa na mpango wa kuachana na Brentford kwenye dirisha hili la usajili huku klabu hiyo ikigomea ofa ya Pauni 25 milioni kutoka Newcastle United.
Wissa alisafiri na timu hadi Ureno ambako kuna mechi ya kirafiki dhidi ya Gil Vicente. Lakini, staa huyo alirudi London baada ya kuelezwa juu ya ishu yake ya uhamisho.
Kinachoelezwa ni kwamba Brentford iligomea ofa ya Pauni 25 milioni ya kuhusu mshambuliaji huyo, ambapo Newcastle imeonyesha dhamira ya kumsajili baada ya kumkosa mkali wa Eintracht Frankfurt, Hugo Ekitike, ambaye atajiunga na Liverpool.
Wissa sasa anatarajia kufanya mazungumzo na mkurugenzi wa soka wa Brentford, Phil Giles ili kufahamu hatima yake.
Timu tatu wapinzani wa Brentford kwenye Ligi Kuu England, Newcastle, Nottingham Forest na Tottenham zote zimeonyesha dhamira ya kunasa saini ya mkali huyo wa kimataifa wa DR Congo.
Kinachoelezwa hadi makubaliano binafsi yameshafikiwa, huku ishu ya kujiunga na Newcastle na Spurs haionekani kuwa tatizo kwa mchezaji huyo kutokana na timu zote kumpa fursa ya kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao.
Wissa amebakiza miezi 12 kwenye mkataba wake wa sasa na kuna kipengele cha kuongeza mwaka mmoja zaidi. Mabosi wa Brentford wanataka kuanzisha mazungumzo ya kuhusu dili jipya, lakini shida ni kwamba wanatambua staa huyo atataka kuondoka.
Wissa alijiunga na Brentford mwaka 2021 baada ya timu hiyo kupanda Ligi Kuu England. Amecheza mechi 149 kwenye kikosi hicho na kufunga mabao 49 na asisti 13.
Fowadi ya Brentford inazidi kupanguka kwani Bryan Mbeumo tayari ameshajiunga na Manchester United kwa ada ya Pauni 65 milioni. Na imempoteza pia kiungo, Christian Norgaard, aliyetimkia Arsenal na kocha wao Thomas Frank amekwenda Tottenham.