Wembanyama aongoza NBA 2026, Lebron akosekana
Muktasari:
- Kadri msimu wa NBA 2025–26 unavyofikia tamati na mchujo (playoffs) kuanza, orodha mpya ya wachezaji bora 20 imeibua mjadala mkubwa hasa baada ya jina la gwiji LeBron James kukosekana.
NEW YORK, MAREKANI: KATIKA mpira wa kikapu, mjadala wa nani ni mchezaji bora zaidi duniani haujawahi kufika mwisho na mara nyingi kila zama huja na nyota wake lakini ni wachache sana wanaotawala mjadala huo kwa muda mrefu.
Kadri msimu wa NBA 2025–26 unavyofikia tamati na mchujo (playoffs) kuanza, orodha mpya ya wachezaji bora 20 imeibua mjadala mkubwa hasa baada ya jina la gwiji LeBron James kukosekana.
Kwa miaka mingi, majina kama Michael Jordan, Kobe Bryant na Kareem Abdul-Jabbar yalitawala mjadala wa wachezaji bora wa muda wote.
Hata hivyo, kadri muda unavyosonga mbele, kizazi kipya kimeanza kujitokeza kwa nguvu, kikibadilisha taswira ya mchezo huo kwa kasi, mbinu mpya na ushindani mkubwa zaidi.
Katika miaka ya sasa, mafanikio hayapimwi tu kwa pointi au mataji, bali pia kwa kiwango cha mchezaji katika timu, ubora wake katika msimu mzima na uwezo wa kubeba presha katika michezo mikubwa.
WEMBANYAMA ANAONGOZA, SGA NA JOKIC WAFUATIA
Kinara wa orodha hiyo ni Victor Wembanyama wa San Antonio Spurs ambaye ameonyesha kiwango cha juu sana msimu huu. Mchezaji huyo kijana kutoka Ufaransa sio kwamba ni mrefu pekee pia ni mwenye uwezo wa kulinda na ana ustadi mzuri sana wa kushambulia unaomfanya kuwa tishio.
Wembanyama ameibuka kama sura mpya ya NBA, akiwa na uwezo wa kubadili matokeo ya mchezo. Uwezo wake wa kuzuia, kufunga pointi nyingi na kucheza kwa akili umeifanya Spurs kuwa timu ya kuangaliwa kwa karibu katika mchujo.
Nafasi ya pili inashikiliwa na Nikola Jokic wa Denver Nuggets, ambaye anaendelea kuthibitisha ubora wake kama mmoja wa wachezaji kamili zaidi kuwahi kutokea. Jokic ana uwezo wa kusoma mchezo, kutoa pasi za hatari na kufunga kwa ufanisi mkubwa.
Katika nafasi ya tatu yupo Luka Doncic wa Los Angeles Lakers ambaye ameendelea kung’ara kama mmoja wa wafungaji bora duniani. Uwezo wake wa kudhibiti mchezo na kubeba timu katika nyakati ngumu unamfanya kuwa mchezaji muhimu sana kwa Lakers.
Nafasi ya nne inachukuliwa na Shai Gilgeous-Alexander wa Oklahoma City Thunder ambaye ameiongoza timu yake kwa mafanikio makubwa msimu huu. Ubora wake na uwezo wa kufunga kwa ufanisi vimemuweka katika mbio za MVP.
NYOTA WENGINE WANG’ARA
Katika nafasi ya tano yupo Giannis Antetokounmpo ambaye licha ya changamoto ndani ya timu yake bado anaendelea kuwa miongoni mwa wachezaji bora zaidi duniani. Majina mengine yanayokamilisha kumi bora ni pamoja na Jaylen Brown, Anthony Edwards, Kawhi Leonard, Cade Cunningham na Stephen Curry.
Wachezaji hawa wamekuwa nguzo muhimu katika timu zao, wakionyesha kiwango cha juu cha ushindani na ubora katika msimu mzima.
Baadhi yao ni vijana wanaochipukia huku wengine wakiwa ni wazoefu wanaoendelea kuthibitisha ubora wao.
LEBRON NJE YA ORODHA
Kukosekana kwa LeBron James katika orodha hii kumezua mjadala mkubwa sana. Wapo wanaoamini kuwa huu ni mwanzo wa mwisho wa enzi yake, huku wengine wakisisitiza kuwa bado ana mchango mkubwa, hasa katika michezo mikubwa.
Ni ukweli kwamba msimu huu LeBron amekuwa si chaguo la kwanza katika safu ya ushambuliaji wa Lakers, hali ambayo imeathiri nafasi yake katika viwango vya sasa vya ubora.
Hata hivyo, haiwezi kupuuzwa kwamba LeBron ni mmoja wa wachezaji wakubwa zaidi katika historia ya mchezo huu, akiwa na rekodi na mafanikio mengi.
KIZAZI KIPYA CHATAWALA
Kwa ujumla, orodha hii inaonyesha wazi kuwa NBA ipo katika kipindi cha mpito wa kizazi. Nyota vijana kama Wembanyama, Doncic na Gilgeous-Alexander sasa wanachukua nafasi ya wakongwe na kuleta ushindani mpya.
Mabadiliko haya yanaifanya ligi kuwa ya kuvutia zaidi, huku kila msimu ukileta hadithi mpya na ushindi mkubwa zaidi.
Mashabiki wa mpira wa kikapu sasa wanashuhudia kizazi kipya kilichojaa vipaji, kasi na ubunifu wa hali ya juu. Swali linalobaki ni nani atadumu kileleni na kuandika historia mpya katika miaka ijayo.
Wakati mchujo ukiendelea,macho yote yataelekezwa kwa nyota hawa kuona nani atakayethibitisha ubora wake pale panapohitajika zaidi uwanjani.