Waarabu wabipu kwa Fernandes, wapigiwa

Muktasari:
- Ripoti zinafichua kwenye kikosi cha Man United kuna wachezaji wanne ambao hawatauzwa kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi, lakini wengine wote waliobaki kama kutakuwa na ofa nzuri, watapigwa bei.
MANCHESTER,ENGLAND: MIAMBA ya soka ya Saudi Arabia, Al-Hilal ipo tayari kuweka mkwanja wa maana mezani kwa ajili ya kuishawishi Manchester United iwauzie kiungo wao matata, Bruno Fernandes dirisha lijalo la majira ya kiangazi - lakini ilichojibu klabu hiyo ya Old Trafford ni Mreno huyo hauzwi.
Ripoti zinafichua kwenye kikosi cha Man United kuna wachezaji wanne ambao hawatauzwa kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi, lakini wengine wote waliobaki kama kutakuwa na ofa nzuri, watapigwa bei.
Mastaa hao ni Fernandes, Harry Maguire, Amad Diallo na Patrick Dorgu.
Man United haijakaa vizuri sana kifedha hivyo itahitaji kuuza baadhi ya wachezaji wake ili kupata pesa za kusajili wakali wapya.
Tayari kuna baadhi ya mastaa wameshafahamu wameshatanguliza mguu mmoja nje kwenye mlango wa kutokea.
Fernandes amekuwa kwenye kiwango bora sana msimu huu huko Old Trafford na ndio maana anavutia ofa kutoka kwenye timu mbalimbali. Klabu hiyo ya Saudi Pro League ina pesa ya kutosha na mwaka jana ilijaribu kumsajili Mohamed Salah, lakini aliamua kubaki Liverpool na sasa wanapambana kumchukua Fernandes.
Kinachoelezwa ni kulikuwa na mawasiliano baina ya pande hizo mbili mwaka jana kabla ya Fernandes kusaini mkataba mpya unaomfanya abaki Manchester hadi 2027.
Ripoti za kutoka Mashariki ya Kati zinadai mawakala wa Fernandes walikuwa na mazungumzo na mabosi wa Al-Hilal, Jumatatu.
Hata hivyo, hakuna ofa yoyote rasmi kutoka Al-Hilal huku Man United ikisisitiza kiungo wao huyo hauzwi kwa gharama yoyote baada ya kuchangia karibia mabao 40 msimu huu, akifunga 19 na kuasisti 18.
Mwezi uliopita, Fernandes alihusishwa na Real Madrid na Kocha wa Man United, Ruben Amorim alizuia uhamisho huo kutokea, aliposema: “Hapana, hilo haliwezi kutokea. Haendi kokote na nilishamwambia!
“Namtaka Bruno hapa kwa sababu nataka kushinda ubingwa wa Ligi Kuu England tena, hivyo tunahitaji wachezaji bora waendelee kubaki na sisi. Ana miaka 30, lakini bado kijana kwa sababu ana uwezo wa kucheza mechi 55 kila msimu. Kati ya asisti na mabao, anafikisha walau 30, hivyo ni aina ya mchezaji tunayemtaka, hivyo haendi popote.”