Vinicius Jr, Madrid waanza kujadili mkataba mpya
Muktasari:
- Taarifa zinaeleza Vinicius aligoma kusaini mkataba mpya, na alikuwa tayari kuondoka ikiwa Alonso angeendelea kusalia katika kikosi hicho kwa sababu alikuwa anaona hampi nafasi kubwa ya kucheza kikosi cha kwanza.
REAL MADRID wameanza mazungumzo ya kumuongeza mkataba wa nyota wa kimataifa wa Brazil, Vinicius Junior, 25, ikiwa ni siku chache baada ya kuondoka kocha Xabi Alonso ambaye inadaiwa kuwa hakuwa katika maelewano mazuri na supastaa huyo.
Taarifa zinaeleza Vinicius aligoma kusaini mkataba mpya, na alikuwa tayari kuondoka ikiwa Alonso angeendelea kusalia katika kikosi hicho kwa sababu alikuwa anaona hampi nafasi kubwa ya kucheza kikosi cha kwanza.
Hata hivyo, Vinicius aliendelea kuwa mmoja wa wachezaji muhimu zaidi ndani ya kikosi cha Real Madrid kutokana na kasi, ubunifu na mchango mkubwa aliokuwa akiutoa katika mabao.
Mabosi wa timu hiyo wanataka kumpa mkataba wa muda mrefu zaidi ili kuzima kabisa tetesi zinazomhusisha na baadhi ya timu za Ulaya na Saudi Arabia. Vinicius anataka mshahara sawa na Kylian Mbappe ambao ni takriban Euro 600,000 kwa wiki ili kusaini mkataba mpya. Mkataba wa sasa unaisha 2027.
Davide Frattesi
NOTTINGHAM FOREST imeongeza kasi katika juhudi za kumsajili kiungo wa Inter Milan na Italia, Davide Frattesi, 26, kwenye dirisha hili la usajili. Frattesi amekuwa mmoja kati ya viungo wanaofanya vizuri Serie A, lakini hivi karibuni amekuwa hapati nafasi ya kutosha kikosi cha kwanza jambo linalomfanya aangalie uwezekano wa kuondoka, na inadaiwa kuwa Ligi Kuu England ni moja kati ya sehemu ambazo anahitaji kucheza. Mkataba wake unaisha 2027.
Dani Ceballos
ASTON VILLA imeanza kumuweka kwenye orodha ya mastaa inaowataka kiungo wa Real Madrid na timu ya taifa ya Hispania, Dani Ceballos, 29, baada ya kushindwa kufanikisha dili la Conor Gallagher aliyejiunga na Tottenham hotspur. Ceballos ambaye amekuwa akipata nafasi ndogo katika kikosi cha Real Madrid, anaonekana kuwa tayari kwa changamoto mpya itakayompa muda mwingi wa kucheza na Villa inaamini uzoefu wake utaipa mafanikio zaidi.
Alejo Veliz
TOTTENHAM Hotspur ipo tayari kusikiliza maombi ya timu yoyote inayohitaji huduma ya mshambuliaji raia wa Argentina, Alejo Veliz, 22, ambaye yupo kwa mkopo Rosario Central. Spurs imeanza mazungumzo na Bahia ya Brazil ili kumuuza baada ya kuona hana nafasi katika mipango ya muda mrefu ya timu. Veliz alijiunga na Spurs kwa matarajio makubwa, lakini kukosa muda wa kucheza kumefanya ifikirie njia mbadala.
Federico Chiesa
JUVENTUS imeamua kupunguza kasi ya kutaka kumsajili upya mshambuliaji wa Liverpool na timu ya taifa ya Italia, Federico Chiesa, 28. Licha ya staa huyo kuwahi kucheza kwa kiwango bora katika kikosi hicho kabla hajaenda Liverpool, taarifa zinaeleza mabosi wa timu hiyo kwa sasa hawaoni tena kipaumbele cha kumsajili, wakizingatia masuala ya kifedha pamoja na mwelekeo wa kujenga kikosi chenye idadi kubwa ya wachezaji wadogo.
Harry Maguire
MANCHESTER United imekataa ofa kadhaa zilizowasilishwa na timu za Ligi Kuu England pamoja na AC Milan ya Italia kwa ajili ya beki wa kimataifa wa England, Harry Maguire, 32, katika dirisha hili la usajili la Januari. Licha ya tetesi za muda mrefu kuhusu mustakabali wake, Man United imeamua kumbakisha Maguire kutokana na umuhimu wake katika kikosi. Pia inasumbuliwa na majeraha kadhaa. Mkataba unamalizika msimu huu.
Ricardo Pepi
FULHAM inaendelea kufuatilia kwa karibu hali ya mshambuliaji wa PSV Eindhoven na timu ya taifa ya Marekani, Ricardo Pepi, 23, licha ya mchezaji huyo kupata jeraha la kuvunjika mkono mwezi huu. Pepi alikuwa mfungaji muhimu wa mabao PSV kabla ya kuumia, jambo lililoifanya Fulham iamini kwamba anafaa kuwa sehemu ya mipango yake ya muda mrefu. Mkataba anamaliza 2030.
Kobbie Mainoo
KIUNGO wa Manchester United, Kobbie Mainoo, 20, bado anafikiria kuondoka katika dirisha hili ikiwa ataendelea kutopata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza. Kwa sasa Napoli ndio inaongoza mbio za kutaka kumsajili staa huyo ambaye inamtaka kwa mkopo wa nusu msimu utakaokuwa na kipengele cha kumnunua mazima ikiwa itaridhishwa na kiwago chake ifikapo mwisho wa msimu.