Vinicius JR kuikosa Argentina ya Messi

MADRID, HISPANIA. WINGA wa Real Madrid, Vinicius Junior alitoka nje ya uwanja akiwa anachechemea kwenye mechi ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia, akiicha Brazil ikipokea kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Colombia.

Lakini, kuna shaka kwamba huenda akakosa mechi inayofuata ya kufuzu dhidi ya Argentina inayoongozwa na Lionel Messi katika mchezo huo utakaochezwa Jumanne.

Supastaa huyo alitengeneza nafasi ya bao lililowekwa kimiani na Gabriel Martinelli dakika ya nne katika mechi yake ya mwisho ya kimataifa, lakini nafasi yake ilichukuliwa na Joao Pedro baada ya kutolewa nje. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 amekuwa akikabiliwa na tatizo la maumivu ya misuli ya paja msimu huu, huku maumivu mengine sehemu ya paja yakiibuka.
Vinicius hatalazimishwa kucheza dhidi ya Argentina kutokana na tatizo hilo na uongozi wa Madrid unaendelea kufuatilia kwa karibu.

Baada ya mchezo kumalizika alielezea kwa kina kuhusu tatizo hilo: “Jeraha hili linafanana na lile lililopita. Nilikuwa na uvimbe na nilihisi baadaye kidogo. nitafanya vipimo nione itakuaje. Nadhani ni ngumu (kucheza dhidi ya Argentina) kwa sababu madaktari walisema. Tutafanya juu chini kuona kama kuna uwezekano.”

Mabao mawili ya nyota wa Liverpool, Luis Diaz yaliifanya Colombia kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Brazil, na kufuatia kichapo hicho Brazil ipo nafasi ya tano kwenye orodha ya timu za Shirikishp la Soka Amerika Kusini (Conmebol) zinazowania nafasi ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 ambapo imekusanya pointi saba baada ya michezo mitano.