Van Dijk aonya gemu ya Arsenal
Muktasari:
- Van Dijk alizungumza hilo akifikiria kipute cha Jumapili hii wakati Liverpool itakapokipiga na Arsenal kwenye mchakamchaka wa Ligi Kuu England, huku timu hizo zote mbili zikishinda mechi zao mbili za kwanza.
LIVERPOOL, ENGLAND: BEKI wa kati na nahodha wa Liverpool, Virgil van Dijk amewaonya wachezaji wenzake kwenye kikosi hicho kwamba wanapaswa kukaza buti kama kweli wanataka kutetea taji la Ligi Kuu England msimu huu.
Van Dijk alizungumza hilo akifikiria kipute cha Jumapili hii wakati Liverpool itakapokipiga na Arsenal kwenye mchakamchaka wa Ligi Kuu England, huku timu hizo zote mbili zikishinda mechi zao mbili za kwanza.
Nahodha huyo ameibua wasiwasi kwa namna Liverpool inavyoruhusu mabao, ambapo kwenye mechi mbili zilizocheza hadi sasa imesharuhusu mabao manne, ilipomenyana na Bournemouth na Newcastle United na hilo ndilo linamtia hofu.
Mdachi huyo alisema Liverpool ndiyo inayopaswa kuwa na wasiwasi mkubwa kuliko Arsenal, ambayo imetumia karibu Pauni 300 milioni kwenye dirisha hili la usajili, huku lengo likiwa ni kuwapiku mabingwa hao watetezi kwenye ligi.
Van Dijk alisema: “Natazama kwenye jambo hilo na naona ulazima wa kutaka kuboresha kiwango chetu ili kutetea ubingwa. Timu nyingine zimeboresha vikosi vyao msimu huu, lakini ni juu yetu kung'ang'ania mwenendo wa kushinda mechi zetu na si vinginevyo.
“Miaka mingine ambayo tulifanikiwa, hakutazama timu nyingine. Sina cha kusema zaidi, lakini timu zote kwenye Ligi Kuu England kwa maoni yangu, zote ni nzuri. Tunacheza kwenye timu bora sana na yenye kocha bora na tutakuwa washindani kwenye Ligi Kuu England kwa miaka mingi.”
Van Dijk alitaka timu hiyo kuboresha viwango vyao kwenye kucheza mipira ya kutenga ambayo ilikuwa changamoto kubwa kwenye mechi dhidi ya Newcastle.