Valverde azichapa na Tchouameni, akimbizwa hospitali
Muktasari:
- Kituo cha TV cha El Chiringuito, kimeripoti kuwa kocha wa muda, Alvaro Arbeloa, alilazimika kuongozana na Valverde hospitali ambapo mchezaji huyo alidaiwa kuhitaji kushonwa. Mkutano wa dharura umefanyika klabuni hapo kujaribu kunusuru msimu ambao unazidi kusambaratika.
MADRID, HISPANIA: KLABU ya Real Madrid imeingia kwenye msukosuko baada ya kiungo wao nyota, Federico Valverde, kukimbizwa hospitali kufuatia mapigano ya mara ya pili ndani ya uwanja wa mazoezi na mchezaji mwenzake, Aurelien Tchouameni.
Ripoti kutoka nchini Hispania zinasema kuwa, ugomvi huo ulioanza tangu Jumatano, uliendelea hadi Alhamisi, ambapo Valverde alipata jeraha lililohitaji matibabu ya haraka. Gazeti la Marca limeelezea tukio hilo kama ‘zito sana,’ likidai kuwa wachezaji hao walizichapa ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo.
Inasemekana kuwa mvutano ulianza baada ya mchezaji mmoja kumchezea rafu mwenzake wakati wa mazoezi huko Valdebebas. Hali ilikuwa mbaya zaidi Alhamisi baada ya Valverde kukataa kupeana mikono na Tchouameni, jambo lililozua mapigano mengine ndani ya jengo kuu la klabu.
Kituo cha TV cha El Chiringuito, kimeripoti kuwa kocha wa muda, Alvaro Arbeloa, alilazimika kuongozana na Valverde hospitali ambapo mchezaji huyo alidaiwa kuhitaji kushonwa. Mkutano wa dharura umefanyika klabuni hapo kujaribu kunusuru msimu ambao unazidi kusambaratika.
Klabu hiyo inayoelekea kumaliza msimu wa pili mfululizo bila taji, imekumbwa na mfululizo wa matukio ya utovu wa nidhamu. Inasemekana takriban wachezaji sita hawazungumzi na kocha Arbeloa.
Beki Antonio Rudiger anadaiwa kumpiga kofi beki Alvaro Carreras, ingawa alishaomba radhi huku Kylian Mbappe akikabiliwa na shinikizo kubwa baada ya kuonekana akistarehe na mwanamitindo Ester Exposito wakati akiwa majeruhi. Zaidi ya mashabiki milioni 32 wamesaini ombi wakimtaka aondoke klabuni hapo.
Mtikisiko huu unakuja wakati Real Madrid ikijiandaa kuvaana na mahasimu wao Barcelona wikendi hii katika dabi ya El Clasico kule Camp Nou. Ikiwa Madrid haitashinda mchezo huo, itairuhusu Barcelona kutawazwa kuwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Hispania (La Liga).
Huku wakiwa wameshatolewa kwenye Ligi ya Mabingwa na Bayern Munich mwezi uliopita, Real Madrid sasa inapambana na vita ya ndani inayoweza kusababisha mabadiliko makubwa klabuni hapo msimu ujao.