Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UEFA CL Bayern vs PSG, vita ya mwisho Allianz Arena

Muktasari:

  • Ni mechi ya marudiano na Bayern inaikaribisha PSG iliyotoka kuichapa mabao 5-4 mkondo wa kwanza na inataka kuutumia uwanja wa nyumbani kulipa kisasi na kufuzu fainali.

MUNICH, UJERUMANI: Leo, Jumatano dunia itasimama kushuhudia mechi nyingine ya kuwania kufuzu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya wawili wa soka la Ulaya, Bayern Munich na Paris Saint-Germain, katika dimba la Allianz Arena.

Ni mechi ya marudiano na Bayern inaikaribisha PSG iliyotoka kuichapa mabao 5-4 mkondo wa kwanza na inataka kuutumia uwanja wa nyumbani kulipa kisasi na kufuzu fainali.

Takwimu zinaonyesha mabingwa hao wa Bundesliga msimu huu wa 2025/26  imekuwa na wastani wa kufunga  mabao kuanzia matatu nyumbani huku kijumla ikifunga 113 katika mashindano yote, kiwango bora zaidi.

Hata hivyo, historia sio rafiki kwa Bayern ambayo katika hatua hii ikifungwa mkondo wa kwanza, imekuwa ikishindwa kupindua meza na hivyo kuongeza presha katika kikosi hicho.

Kocha Vincent Kompany ana kazi kubwa ya kujipanga na kurekebisha makosa yaliyotokea katika mechi ya kwanza ugenini.

PSG ambayo itakuja kwa kujiamini, ina kazi ya kuhakikisha haiipi nafasi Bayern ya kupindua matokeo na hivyo itacheza kwa kujilinda zaidi na kushambulia kwa kushtukiza.

PSG imekuwa na rekodi nzuri sana katika hatua za mtoano, hasa wanapopata ushindi katika mchezo wa kwanza na mara nyingi inalinda ushindi huo, jambo linalowapa matumaini mashabiki.

Kocha Luis Enrique ambaye anajulikana kwa uwezo wake wa kusimamia mechi kubwa na kufanya maamuzi sahihi katika nyakati muhimu, atakuwa na jukumu la kuhakikisha timu yake inacheza kwa nidhamu, inazuia makosa ya kizembe na inatumia vizuri nafasi chache zitakazopatikana.

PSG pia wana silaha kubwa katika safu yao ya ushambuliaji inayoongozwa na Ousmane Dembele mwenye mabao 10 na asisti sita kwenye ligi na mabao sita na asisti mbili kwenye michuano hii.


VITA KIUFUNDI

Bayern inatarajiwa kuingia uwanjani kwa lengo la kutafuta mabao ya mapema yatakayoipa nguvu ya kumaliza mechi hiyo.

Inapenda kushambulia kutoka pembeni na mabeki wao hupanda juu kusaidia mashambulizi huku mawinga wakitumia kasi kuvunja ulinzi wa wapinzani.

Hata hivyo, mbinu hii inaacha nafasi nyuma, jambo ambalo linaweza kuwa hatari  dhidi ya timu yenye kasi kama PSG ambayo inatarajiwa kucheza kwa tahadhari zaidi, wakilinda faida yao, pia kushambulia kwa kushtukiza kwa kuwatumia washambuliaji wake wenye kasi.

Kiungo cha kati kitakuwa eneo muhimu sana katika mchezo huu, kwani ndicho kitakachoamua nani anadhibiti mwelekeo wa mchezo.

Timu itakayoweza kumiliki mpira kwa utulivu na kupunguza makosa ina nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi.

Pia, ubora wa kumalizia nafasi utakuwa muhimu, kwani nafasi zinaweza kuwa chache lakini zenye thamani kubwa.


HALI YA VIKOSI

Bayern inaonekana kuwa katika hali nzuri kwa jumla, licha ya kukosekana kwa baadhi ya wachezaji kutokana na majeraha.

Nyota wao Harry Kane mwenye mabao 33 na asisti tano kwenye Bundesliga mabao 13 na asisti mbili  katika Ligi ya Mabingwa ndiye tegemeo kubwa katika safu ya ushambuliaji, akiwa katika kiwango bora kabisa na akiwa na uwezo wa kubadili matokeo wakati wowote.

Uzoefu wa Manuel Neuer langoni na Joshua Kimmich katikati ya uwanja utakuwa muhimu sana katika kudhibiti mchezo na kuhakikisha timu inacheza kwa utulivu.

Hata hivyo, kukosekana kwa baadhi ya wachezaji kama Serge Gnabry na Raphael Guerreiro (majeraha)  kunaweza kupunguza machaguo zaidi kwenye kikosi hicho.

Kwa upande wa PSG, pigo kubwa ni kukosekana kwa Achraf Hakimi (majeraha) ambaye ni muhimu sana katika mfumo wao wa kucheza, kunaweza kuathiri usawa wa timu, hasa katika upande wa kulia wa ulinzi na mashambulizi.

Hata hivyo, PSG bado wana kikosi chenye ubora mkubwa, wakiwa na wachezaji hatari kama Ousmane Dembele na Khvicha Kvaratskhelia ambao wanaweza kuamua matokeo ya mchezo kwa ubunifu wao.

Kwa jumla, timu zote zina vikosi vyenye uwezo mkubwa na ni nani atakayekuwa makini zaidi ndiye atakayepata tiketi ya kwenda fainali.