Thamani ya vikosi England hii hapa

Muktasari:
- Kwa mujibu wa transfermarkt, kikosi cha kocha Pep Guardiola, Manchester City kinashika namba moja kwa kuwa na thamani ya Euro 1.35 bilioni. Chelsea haipo mbali sana, ikiwa na kikosi chenye thamani ya Euro 1.21 bilioni.
LONDON, ENGLAND: KLABU za Big Six za Ligi Kuu England hadi sasa zinaundwa na vikosi vya thamani ya Pauni 5 bilioni baina yao huku pengo la thamani ya vikosi kwenye ligi hiyo likizidi kutanuka.
Kwa mujibu wa transfermarkt, kikosi cha kocha Pep Guardiola, Manchester City kinashika namba moja kwa kuwa na thamani ya Euro 1.35 bilioni. Chelsea haipo mbali sana, ikiwa na kikosi chenye thamani ya Euro 1.21 bilioni.
Liverpool na Arsenal ziko nyuma, zikiwa na vikosi vyenye thamani Euro 1.09 bilioni na Euro 1.01 bilioni mtawalia. Licha ya miaka kadhaa ya kutumia pesa nyingi kwenye usajili, kikosi cha Manchester United kinashika namba tano, kikiwa na thamani ya Euro 818 milioni.
Wakati huo, kwenye upande mwingine wa orodha hiyo, kuna timu tatu zilizopanda daraja msimu huu, kwamba ndizo zenye vikosi vyenye thamani ndogo zaidi hadi sasa. Mabingwa wa Championship, Leeds United kikosi chao kina thamani ya Euro 211 milioni, kikijiandaa kupambana kwenye Ligi Kuu England baada ya kukosekana kwa miaka miwili.
Burnley ipo nyuma ikiwa na thamani ya Euro 187 milioni, wakati Sunderland thamani ya kikosi chake ni Euro 137 milioni, kitu ambacho kinawafanya wadau wengi kuamini watakabiliwa na vita kali kubaki kwenye Ligi Kuu England hadi msimu ujao.
Hata hivyo, thamani za vikosi hivyo vya Ligi Kuu England vinaweza kubadilika hadi hapo dirisha la usajili la majira ya kiangazi litakapofungwa kwa sababu kuna mastaa wapya wataingia huku wengine wakitimka.