Ten Hag atoa onyo kwa wapinzani

MANCHESTER, ENGLAND. KOCHA wa Manchester United, Erik ten Hag, amekiri timu yake italeta ushindani kwenye mbio za kuwania ubingwa msimu ujao, kwasababu wapo katika muelekeo mzuri.

Man United ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu England kwa tofauti ya pointi 16 dhidi ya vinara Arsenal baada ya kupoteza pointi tano katika mechi mbili za mwisho. Man United ilipokea kichapo cha mabao 7-0 dhidi ya Liverpool, baadaye ikalizimishwa suluhu ilipochezwa dhidi ya Southampton wikiendi iliyopita.

Aidha Ten Hag ameuanza msimu wake wa kwanza kwa kishindo, Man United ikibeba ubingwa wa Kombe la Carabao huku wakiwa na matumaini ya kumaliza msimu katika nafasi za juu yaani 'Top Four'

Mara ya mwisho Man United kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England ilikuwa msimu wa 2012-2013 chini ya Sir Alex Ferguson, lakini Ten Hag anaamini timu yake imebadilika kwasababu wachezaji wake wamejituma sana.

"Matunda yameanza kuonekana, lakini bado kuna pengo jukumu letu ni kuliziba, tunachotaka ni kushinda kila mechi, haijalishi tumecheza na timu gani, kila mechi tulizocheza msimu huu tumejaribu kushinda, tumezifunga timu zote kubwa kwenye ligi, tuna uwezo wa kufanya mambo makubwa, muhimu tuendelee mwendo wetu huu huu, naamini tunaweza," alisema Ten Hag Wakati huohuo Man United itakosa huduma ya kinda wake Alejandro Garnacho baada ya kuumia wikiendi iliyopita kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Southampton, vile vile itaendelea kumkosa kiungo wao Christian Eriksen ambaye aliumia kweenye mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Reading.

Uongozi wa Man United umechukizwa na maamuzi ya marefa msimu huu ambayo yamesababisha wachezaji wao kuumia, Casemiro akilimwa kadi nyekundu. Sasa kiungo huyo atakosa mechi nne kwasababu hiyo ni kadi yake ya pili nyekundu tangu alipotua Old Trafford akitokea Real Madrid.