Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ten Hag afutwa kazi Bayer Leverkusen

TEN Pict

Muktasari:

  • Mdachi huyo aliyewahi kuinoa Manchester United alijiunga na klabu hiyo ya Bundesliga, Mei mwaka huu baada ya miezi saba ya kutokuwa na kazi na sasa amefukuzwa kazi baada ya siku 62 tu za kuwa kazini.

MUNICH, UJERUMANI: KOCHA, Erik ten Hag amefutwa kazi huko Bayer Leverkusen.

Mdachi huyo aliyewahi kuinoa Manchester United alijiunga na klabu hiyo ya Bundesliga, Mei mwaka huu baada ya miezi saba ya kutokuwa na kazi na sasa amefukuzwa kazi baada ya siku 62 tu za kuwa kazini.

Katika mechi yake ya kwanza ya kiushindani, Ten Hag alishuhudia timu yake ikishinda 4-0 dhidi ya timu ya daraja la nne SG Sonnenhof Großaspach kwenye mechi ya raundi ya kwanza ya DFB-Pokal.

Hata hivyo, kwenye Bundesliga, Leverkusen ilichapwa 2-1 na Hoffenheim kabla ya kutoka sare ya 3-3 dhidi ya Werder Bremen iliyokuwa na wachezaji 10 uwanjani.

Na mabosi wa klabu wameamua kumfuta kazi kocha huyo mwenye umri wa miaka 55, ambaye mkataba wake ulikuwa unafika ukomo 2027.

Kwenye taarifa yao fupi iliyotolewa kwenye mtandao wa kijamii ilibainisha: “Bayer 04 Leverkusen imeachana na kocha wake mkuu Erik ten Hag kwa haraka. Mazoezi sasa yatakuwa chini ya makocha wasaidizi kwa kipindi hiki.”

Ten Hag alitua kwenye klabu hiyo kuchukua mikoba ya Xabi Alonso, ambaye kwenye msimu wa 2023/24 aliweka rekodi ya kuingoza Leverkusen kucheza msimu mzima bila ya kupoteza mechi kwenye Bundesliga ikibeba taji hilo sambamba na la DFB-Pokal.

Lakini, sasa kocha huyo Mhispaniola amekwenda kujiunga na Real Madrid msimu huu.

Baada ya mechi ya Bremen, Leverkusen inashika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi ya Bundesliga na kocha Ten Hag aliwaambia wachezaji wake kwamba hawapo tayari kwa msimu huu, alisema: “Wachezaji hawapo sawa. Tuna timu mpya na si wachezaji wote wapo fiti kucheza. Tunahitaji kupambana zaidi na kuwa fiti ili kufikia viwango.”

Kuondolewa kwake kunafanya kuwa kocha wa tatu wa zamani wa Man United kufutwa kazi ndani ya wiki moja. Jose Mourinho na Ole Gunnar Solskjaer walifunguliwa milango ya kutokea huko Fenerbahce na Besiktas mtawalia baada ya timu hizo kushindwa kufuzu kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.