Tammy Abraham anukia England, Roma freshi

Muktasari:
- Kwa mujibu wa ripoti Milan haina mpango wa kumsainisha mkataba wa kudumu mshambuliaji huyu baada ya benchi la ufundi kutoridhishwa na kiwango chake, vilevile Roma nayo hayupo kwenye mipango yao kwa msimu ujao.
ROMA ipo tayari kusikiliza ofa kutoka timu nyingine juu ya straika wao raia wa England, Tammy Abraham ambaye msimu huu anacheza kwa mkopo AC Milan.
Kwa mujibu wa ripoti Milan haina mpango wa kumsainisha mkataba wa kudumu mshambuliaji huyu baada ya benchi la ufundi kutoridhishwa na kiwango chake, vilevile Roma nayo hayupo kwenye mipango yao kwa msimu ujao.
West Ham, Wolves na Everton ni miongoni mwa timu zinazotajwa kuimezea mate huduma yake na West Ham ndio inaonekana kuongoza katika mchakato kwani imeshaanza hadi mazungumzo na wawakilishi wake.
Tangu kuanza kwa msimu huu, Tammy mwenye umri wa miaka 27, amecheza mechi 26 za michuano yote na kufunga mabao manane.
Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
Antonee Robinson
MABOSI wa Fulham wamesisitiza kwamba watapokea ofa inayofikia Pauni 40 milioni na kuendelea ikiwa timu yoyote inahitaji huduma ya beki wao wa kushoto raia wa Marekani, Antonee Robinson, 27, ambaye anawindwa na Liverpool na Manchester United kuelekea dirisha lijalo.
Antonee amecheza mechi 58 za michuano yote na kutoa asisti 20.
Mkataba wake unamalizika mwaka 2028.
Jean-Philippe Mateta
MANCHESTER United wameambiwa watoe Pauni 40 milioni ili kuipata saini ya mshambuliaji wa Crystal Palace na Ufaransa, Jean-Philippe Mateta, 27, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Mateta amekuwa katika rada za vigogo wa England tangu dirisha la majira ya baridi mwaka jana kutokana na kiwango bora alichoonyesha tangu kuanza kwa msimu huu. Mkataba wake unamalizika mwaka 2026.
Antoine Semenyo
TOTTENHAM ipo tayari kutoa ofa ya karibia Euro 40 milioni kwenda Bournemouth ili kumsajili winga wa timu hiyo na Ghana, Antoine Semenyo, 25, katika dirisha lijalo.
Tangu kuanza kwa msimu huu Semenyo mwenye umri wa miaka 25, amecheza mechi 30 za michuano yote na kufunga mabao tisa na kutoa asisti tano.
Douglas Luiz
JUVENTUS na Newcastle huenda zikafanya biashara ya mabadilishano ya wachezaji katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ambapo kiungo wa Juve na timu ya taifa ya Brazil, Douglas Luiz, 26, akatimkia Newcastle na Sandro Tonali kwenda upande mwingine. Mkataba wa Luiz unamalizika mwaka 2028 na ule wa Tonali mwaka 2029.
Marcus Thuram
INTER Milan inataka kufanya mazungumzo na wawakilishi wa mshambuliaji wao Marcus Thuram juu ya uwezekano wa kumsainisha mkataba mpya kwani staa huyu wa kimataifa wa Ufaransa, mwenye umri wa miaka 27, kwa sasa ana kipengele cha kuondoka ikiwa timu inayomhitaji italipa Euro 85 milioni.
Thuram kwa sasa ni miongoni mwa mastaa tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Inter.
Arda Guler
EINTRACHT Frankfurt wanachunguza kwa karibu maendeleo ya winga wa Real Madrid na timu ya taifa ya Uturuki, Arda Guler, 20, kabla ya kutuma ofa ya kumsajili kwa mkopo mwisho wa msimu. Guler hapati nafasi kubwa ya kucheza katika kikosi cha Madrid, mara kadhaa amekuwa akitajwa kwamba anataka kuondoka.
Richarlison
EVERTON inafikiria kutuma ofa kwenda Tottenham ili kuipata saini ya mshambuliaji wake wa zamani kutoka Brazil, Richarlison, 27, ambaye amekuwa hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza Spurs na alifikiria kuondoka tangu mwaka jana ambapo alipokea ofa kutoka Saudi Arabia lakini ilishindikana.
Mkataba wa Richarlison unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.