Tajiri kaamua, wafanyakazi wengine kuliwa vichwa united
Muktasari:
- Jumanne ya wiki hii, tovuti ya The Sun iliripoti, Ratcliffe anataka kupunguza wafanyakazi wengine kati ya 100 hadi 200 ikiwa ni njia mojawapo ya kubana matumizi.
MANCHESTER, ENGLAND: TAJIRI na mmiliki mwenza wa Manchester United, Sir Jim Ratcliffe inadaiwa kuwa na hofu timu huenda ikakumbana na hali mbaya ya kiuchumi ikiwa hatochukua jukumu la kuendelea kubana matumizi.
Jumanne ya wiki hii, tovuti ya The Sun iliripoti, Ratcliffe anataka kupunguza wafanyakazi wengine kati ya 100 hadi 200 ikiwa ni njia mojawapo ya kubana matumizi.
Ratcliffe, 72, alilipa Pauni 1 bilioni mwaka jana kwa ajili ya kununua hisa asilimia 27.7 za timu hiyo.
Mara baada ya kununua hisa hizo, alipunguza wafanyakazi 250 kati ya 1,150 Julai mwaka jana jambo lililopingwa vikali na mashabiki wa timu hiyo ambao waliumia zaidi baada ya kocha wao wa zamani, Sir Alex Ferguson kuondolewa mkataba wake wa ubalozi uliokuwa unampa zaidi ya Pauni 1 milioni kwa mwaka.
Kwa mujibu wa tovuti ya The Guardian, Ratcliffe kwa sasa hana chaguo lingine zaidi ya kuvunja mikataba ya baadhi ya wafanyakazi.
ManUnited imepoteza karibia Pauni 300 milioni katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kama hasara na Ratcliffe anaamini anaweza kufidia kiasi hicho ndani ya misimu miwili chini yake.
Vyanzo vya ndani kutoka timu hiyo vinaeleza ingekuwa na hali mbaya ya kiuchumi kwa sasa ikiwa Ratcliffe asingeweka Pauni 240 milioni kama sehemu ya uwekezaji.
Tajiri huyu ambaye ndiye amepewa jukumu la kusimamia shughuli zote za mpira wa miguu, amepanga kuendelea na upunguzaji wa matumizi licha ya kufahamu mashabiki wengi hawavutiwi na hilo.