Szoboszlai amsubiri CR7 ampe jezi, kapewa mwingine
Muktasari:
- Kama ilivyo kwa wachezaji wengi waliowahi kucheza dhidi ya Ronaldo, kiungo huyo wa Hungary, anayechezea Liverpool, Szoboszlai naye alihitaji sana kupata jezi ya Ronaldo baada ya mechi hiyo. Szoboszlai alisubiri nje ya chumba cha kubadilishia nguo cha Ureno ili ampatie Ronaldo jezi yake ya mechi hiyo na kisha na yeye apewe ya CR7.
BUDAPEST, HUNGARY: SUPASTAA, Cristiano Ronaldo ameshindwa kubadilishana jezi na Dominik Szoboszlai baada ya mechi iliyokutanisha timu zao Ureno na Hungary kwenye mchakamchaka wa kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 usiku wa Septemba 9, 2025.
Kama ilivyo kwa wachezaji wengi waliowahi kucheza dhidi ya Ronaldo, kiungo huyo wa Hungary, anayechezea Liverpool, Szoboszlai naye alihitaji sana kupata jezi ya Ronaldo baada ya mechi hiyo. Szoboszlai alisubiri nje ya chumba cha kubadilishia nguo cha Ureno ili ampatie Ronaldo jezi yake ya mechi hiyo na kisha na yeye apewe ya CR7.
Lakini, aliondoka akiwa mwenye huzuni baada ya Ronaldo kumwambia ameshampa mtu mwingine jezi yake.
Hata hivyo, mshindi huyo mara tano wa Ballon d'Or, Ronaldo alionyesha utu wake baada ya kumwambia Szoboszlai atampatia jezi mwezi ujao wakati wa mechi ya marudiano.
Ronaldo alisema: "Nitakupatia jezi yangu ya nyumbani tukikutana Ureno, sawa?"
Picha ya video za wawili hao wakiwa kwenye mazungumzo ilikuwa gumzo mtandaoni.
Shabiki mmoja alisema: "Unapokutana na shujaa wako."
Mwingine akasema: "Mwamba amesema neno. Atalitimiza."
Shabiki wa tatu akaongeza: "Hii ni safi sana kutoka kwa wachezaji hawa. Heshima kubwa kwa vizazi." Pia kuna shabiki alisema: "Kiwango cha juu ndani na nje ya uwanja."
Katika mechi hiyo Ureno ilishinda mabao 3-2 kwenye Kundi F, shukrani kwa mabao ya Bernardo Silva, Joao Cancelo na Ronaldo, aliyefunga kwa mkwaju wa penalti kwenye kipindi cha pili.