Staa Eze abeba matumaini Arsenal
Muktasari:
- Arsenal imefanya matumizi makubwa kwenye dirisha hili la usajili na kuna sura sita mpya kabisa zimewasili kuongeza nguvu huko Emirates.
LONDON, ENGLAND: KIUNGO wa zamani wa Arsenal, Ray Parlour anaamini timu hiyo itafanikiwa kunasa saini ya Eberechi Eze ikiwa ni usajili wao wa mwisho dirisha hili.
Arsenal imefanya matumizi makubwa kwenye dirisha hili la usajili na kuna sura sita mpya kabisa zimewasili kuongeza nguvu huko Emirates.
Noni Madueke, Viktor Gyokeres na Martin Zubimendi ni miongoni mwa mastaa waliojiunga na timu hiyo, huku wengine ni Christian Norgaard, Cristhian Mosquera na Kepa Arrizabalaga.
Lakini, kikosi hicho cha Kocha Mikel Arteta bado hakijamaliza usajili. Arsenal inataka kuongeza winga mmoja kabla ya dirisha kufungwa. Staa wa Crystal Palace, Eze anatazamwa kama mtu mwafaka kama mbadala wa staa wa Real Madrid, Rodrygo, ambaye pia yupo kwenye rada za wakali kao wa Emirates.
Staa wa zamani wa Arsenal, Parlour anaamini timu yake hiyo itafunga dirisha la usajili la majira haya ya kiangazi huko Ulaya kwa kumsajili Eze.
Alisema: “Nadhani ikuna usajili mmoja wa ziada. Sifahamu wamebakiza pesa kiasi gani au sheria zikoje, lakini kama wana pesa za kutosha, Eze atakuwa usajili mzuri.
“Unahitaji kikosi kipana hasa unapocheza Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kombe la FA kwa sababu mechi zinakuwa nyingi. Ndiyo maana nadhani, Eze atafaa.”
Arsenal inapaswa kukamilisha dili la mchezaji huyo kama kweli inataka kuwa timu shindani msimu huu.
Staa huyo Mwingereza anaripotiwa kwenye mkataba wake kimetajwa kiwango cha Pauni 68 milioni kinachotosha kumng’oa huko Crystal Palace, ambako mkataba wake utafika tamati 2027.