Spurs waambiwa mpeni kazi Klopp
Muktasari:
- Spurs kwa sasa inashika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England baada ya kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Nottingham Forest, Jumapili iliyopita.
LONDON, ENGLAND: ALIYEKUWA mmiliki wa Tottenham Hotspur, Lord Alan Sugar amewataka mabosi wa sasa wa timu hiyo kumwajiri kocha Jurgen Klopp ili kwenda kukinoa kikosi hicho.
Spurs kwa sasa inashika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England baada ya kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Nottingham Forest, Jumapili iliyopita.
Kocha wa sasa Spurs, Thomas Frank yupo kwenye presha kubwa sasa baada ya kushinda mara moja tu katika mechi saba zilizopita kwenye ligi.
Lord Sugar, ambaye aliimiliki Spurs kuanzia 1991 hadi 2001, aliandika kwenye X: “Kutokana na utajiri mkubwa iliyonao familia ya Lewis itakuwa ushindi mkubwa kama watamwajiri Jurgen Klopp, Januari.
“Pesa za kutosha kwa wachezaji na kocha mahiri. Sote tunakubaliana kwenye hilo.“
Imeripotiwa kwamba Klopp mkataba wake huko Red Bull unamruhusu kuondoka kwenda kuinoa timu ya taifa ya Ujerumani kama nafasi hiyo itakuwa wazi. Haifahamiki kama kipengele hicho kwenye mkataba wake kinahusiana pia na timu za ngazi ya klabu. Klopp alishinda Bundesliga mara mbili alipokuwa na kikosi cha Borussia Dortmund, kabla ya kwenda kunyakua taji la Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Liverpool.
Wakati tajiri Lord Sugar anaichukua Spurs mwaka 1991, timu hiyo ilikuwa kwenye hatihati ya kufilisika. Lakini, hadi kipindi anaondoka kwenye timu hiyo muongo mmoja baadaye, Spurs imekuwa kwenye hali nzuri ya kiuchumi.