Son atoa chozi akiaga Spurs
Muktasari:
- Mkataba wa mkali huyo wa kimataifa wa Korea Kusini utafika tamati mwishoni mwa msimu huu, lakini sasa ataachana na Spurs kwenye dirisha hili.
LONDON, ENGLAND: STAA na nahodha wa Tottenham Hotspur, Son Heung-min ameshindwa kuvumilia na kumwaga chozi wakati anatangaza kuachana na miamba hiyo ya London.
Mkataba wa mkali huyo wa kimataifa wa Korea Kusini utafika tamati mwishoni mwa msimu huu, lakini sasa ataachana na Spurs kwenye dirisha hili.
Son, 33, amepewa baraka zote za kuondoka kwenye kikosi hicho na bosi Daniel Levy, ikiwa ni miezi miwili tu imepita tangu alipoisaidia timu hiyo kumaliza ukame wa miaka 17 ya bila taji lolote, iliponyakua Europa League.
Kwa hisia kali, Son alisema kwenye mkutano wa waandishi: “Nimeamua kuachana na klabu kwenye dirisha hili. Na nashukuru, klabu imenisaidia kwenye huo uamuzi wangu. Hivyo, napenda kusema hilo kabla ya kuendelea na mengine.”
Staa huyo kipenzi cha mashabiki wa Spurs alijiunga na timu hiyo akitokea Bayer Leverkusen kwenye dirisha la majira ya kiangazi 2015 kwa dili lililokuwa na thamani ya Pauni 22 milioni.
Fowadi huyo alifurahia kila dakika aliyokuwa kwenye kikosi hicho, lakini sasa anaamini ni wakati mwafaka wa kwenda kukabiliana na changamoto mpya.
“Ulikuwa uamuzi mgumu sana kuufanya katika maisha yangu ya soka. Nimekuwa hapa kwa miaka 10 katika klabu hii nzuri, mashabiki wazuri na wenye kumbukumbu za kipekee,” alisema.
Son alikuwa nahodha wa Spurs wakati wanaichapa Manchester United kwenye fainali ya Europa League, Mei mwaka huu. Na mwenyewe anaona ni wakati mwafaka sasa kushusha pazia lake kwenye kikosi hicho cha London na anahusishwa na klabu ya Los Angeles FC. Kwenye kikosi cha Spurs alifunga mabao 173 katika mechi 454.