Solskjaer kibarua kimeota nyasi
Muktasari:
- Uamuzi huo umekuja baada ya timu hiyo kupoteza mbele ya Lausanne ya Uswisi kwenye mchezo wa mchujo wa kushiriki michuano ya Europa Conference League.
BESIKTAS, UTURUKI: KOCHA, Ole Gunnar Solskjaer amefutwa kazi na klabu ya Besiktas ya Uturuki.
Uamuzi huo umekuja baada ya timu hiyo kupoteza mbele ya Lausanne ya Uswisi kwenye mchezo wa mchujo wa kushiriki michuano ya Europa Conference League.
Besiktas ilitoa taarifa isiyozidi maneno 40 iliyosomeka: “Mkataba wetu na kocha Ole Gunnar Solskjaer umesitishwa baada ya uamuzi uliofanywa na kikao cha bodi. Baada ya kikao, mwenyekiti wetu Serdal Adalı, alimshukuru Solskjaer kwa huduma yake. Tunapenda kuufahamisha hilo umma.”
Besiktas imeshindwa kufuzu kucheza mikikimikiki ya Conference League baada ya kipigo cha mabao 2-1 katika mechi mbili ilizokumbana na Lausanne. Kikosi hicho cha Solskjaer kilitoka sare kwenye mechi ya kwanza iliyofanyika Uswisi, ikiwa na matumaini ya kupata ushindi nyumbani, lakini ilipigwa na butwaa baada ya kupoteza 1-0 na hivyo kutupwa nje ya kinyang’anyiro.
Bao lililowatoa nje Besiktas lilifungwa na mchezaji asiyetarajiwa kabisa, kinda wa zamani wa Arsenal, Nathan Butler-Oyedeji. Staa huyo mwenye umri wa miaka 22 alinaswa na klabu hiyo ya Swiss Super League baada ya kuachwa na Arsenal mwishoni mwa msimu uliopita.
Hilo lilikuwa bao lake la kwanza kwenye klabu hiyo. Solskjaer alijiunga na timu hiyo Januari baada ya kuwa nje ya kazi kwa kipindi cha miaka mitatu tangu alipoachana na Man United mwishoni mwa mwaka 2021.
Alionyesha kiwango bora baada ya timu kumaliza nafasi ya nne kwenye msimamo msimu uliopita, ambapo kwenye kikosi chake kulikuwa na huduma ya mastaa kadhaa waliowahi kucheza Ligi Kuu England kama Alex Oxlade-Chamberlain, Arthur Masuaku na Gedson Fernandes.