Snoop aenda kuona timu yake Swansea
Muktasari:
- Rapa huyo mashuhuri duniani aliwasili kwa staili ya kipekee kushuhudia mechi yake ya kwanza ya Championship, akiwa amevaa mavazi ya Swansea City kuanzia juu hadi chini, kabla ya sare ya kusisimua ya bao 1-1.
LONDON, ENGLAND: BOSI wa Preston, Paul Heckingbottom, alitania kwamba aliweza kunusa harufu ya bangi katika korido za uwanjani wakati Snoop Dogg alipohudhuria mechi yake ya kwanza ya moja kwa moja ya Swansea City.
Rapa huyo mashuhuri duniani aliwasili kwa staili ya kipekee kushuhudia mechi yake ya kwanza ya Championship, akiwa amevaa mavazi ya Swansea City kuanzia juu hadi chini, kabla ya sare ya kusisimua ya bao 1-1.
Snoop alinunua hisa katika klabu hiyo ya Wales mwaka jana na kusema kuwa historia ya klabu na jiji iligusa moyo wake. Alisaidia kutangaza jezi ya msimu wa 2025-26 baada ya uwekezaji wake, lakini alisubiri hadi wiki hii kufanya ziara yake rasmi ya kwanza.
Baada ya kutembelea uwanja wa mazoezi Jumatatu na kukutana na wachezaji pamoja na benchi la ufundi, Snoop, mwenye umri wa miaka 54 alifanya mwonekano wake wa kwanza katika Uwanja wa Swansea.com kabla ya pambano la katikati ya wiki la Championship dhidi ya Preston North End. Aliwasili uwanjani akiwa amevaa mavazi meupe kuanzia juu hadi chini, yakiwemo jezi ya Swansea, jaketi na koti, pamoja na suruali nyeupe zenye nembo ya klabu. Mmarekani huyo aliingia pia akiwa amevaa miwani ya jua na kubeba spika.
Alipata muda wa kupiga picha na mashabiki kabla ya mechi kuanza na hata akacheza mpira kidogo uwanjani. Taulo zenye picha yake ziliwekwa kwenye kila kiti cha mashabiki wa nyumbani.
Snoop alipigiwa makofi ya heshima alipofanya mzunguko wa uwanja kabla ya mechi kuanza. Mashabiki walipunga taulo walizopewa bure kumlaki alipokuwa akizunguka pembezoni mwa uwanja. Rapa huyo pia alikutana na gwiji wa EFL, Lee Trundle, ambaye aliichezea Swansea mechi 199 na sasa anafanya kazi klabuni hapo kama kocha wa timu za vijana.
Swansea waliambulia pointi moja kutokana na bao la kusawazisha la dakika za mwisho lililofungwa na Liam Cullen, lililofuta bao la dk26 la Daniel Jebbison. Baada ya mechi, Heckingbottom alisema hakushtushwa na uwepo wa gwiji huyo wa muziki. Alitania: “Kitu pekee nilichogundua tofauti ni harufu ya bangi kwenye handaki kabla ya mechi!”
Snoop aliwaacha wachezaji na wafanyakazi wakiwa wameshangazwa katika ziara yake kwenye uwanja wa mazoezi wa Swansea. Aliimba moja ya nyimbo zake, Drop It Like It’s Hot, ndani ya chumba cha vifaa vya michezo na kuwafanya wote wacheke, huku pia akijaribu kuonyesha ujuzi wake wa soka kwa kuvaa viatu vya mkopo.