Sita Mamelodi waongoza jahazi Afrika Kusini dhidi ya Mexico
Muktasari:
- Broos ameendelea kuamini uti wa mgongo wa Sundowns, timu ambayo imekuwa ikitawala soka la Afrika Kusini na Afrika, akiamini uzoefu na maelewano waliyojenga kwa muda mrefu yanaweza kuisaidia Bafana Bafana kufanya vizuri katika mashindano hayo makubwa.
KOCHA wa Bafana Bafana, Hugo Broos, ameonyesha imani kubwa kwa nyota wa mabingwa wa Afrika Kusini, Mamelod Sundowns, baada ya kuwajumuisha wachezaji sita wa klabu hiyo katika kikosi cha kwanza kilichoshuka dimbani dhidi ya Mexico kwenye mchezo wa ufunguzi wa Kombe la Dunia 2026.
Broos ameendelea kuamini uti wa mgongo wa Sundowns, timu ambayo imekuwa ikitawala soka la Afrika Kusini na Afrika, akiamini uzoefu na maelewano waliyojenga kwa muda mrefu yanaweza kuisaidia Bafana Bafana kufanya vizuri katika mashindano hayo makubwa.
Miongoni mwa nyota wa Sundowns walioanza ni kipa Ronwen Williams, ambaye amekuwa mhimili wa timu ya taifa na klabu yake kutokana na uwezo wake wa kuokoa hatari na kuiongoza safu ya ulinzi.
Katika upande wa kulia wa ulinzi yupo nahodha Khuliso Mudau huku beki wa kushoto akiwa Aubrey Modiba, wote wakitarajiwa kutumia uzoefu wao wa mechi za kimataifa kuizuia Mexico.
Eneo la kiungo liliongozwa na Teboho Mokoena, mmoja wa viungo bora wa Afrika Kusini kwa sasa anayejulikana kwa uwezo wake wa kutawala mchezo, kupiga mipira ya adhabu na kutengeneza nafasi za mabao.
Eneo la ushambuliaji ameanza na Iqraam Rayners, ambaye amekuwa katika kiwango kizuri tangu ajiunge na Sundowns na amepewa jukumu la kuiongoza safu ya ushambuliaji ya Bafana Bafana.
Nyota wa sita kutoka Sundowns aliyeanza ni beki wa kati Grant Kekana, jambo lililoifanya Sundowns kuwa klabu yenye uwakilishi mkubwa zaidi ndani ya kikosi cha kwanza cha Afrika Kusini.
Mbali na nyota hao wa Sundowns, beki wa kati wa Orlando Pirates, Nkosinathi Sibisi, ndiye mchezaji pekee kutoka klabu nyingine ya ndani aliyepata nafasi katika kikosi cha kwanza.
Safu ya ulinzi ilikamilishwa na beki kijana Ime Okon, anayekipiga Hannover ya Ujerumani na ambaye ameanza kujijengea jina kama moja ya vipaji vinavyokuja kwa kasi katika soka la taifa hilo.
Katika nafasi nyingine, Mbekezeli Mbokazi wa Chicago Fire ya Marekani na Yaya Sithole wa Tondela ya Ureno walipewa jukumu la kuongeza nguvu katika safu ya ulinzi iliyoanza na mabeki watatu wa kati na kiungo.
Mshambuliaji wa Burnley, Lyle Foster, naye alipewa nafasi muhimu katika safu ya ushambuliaji kutokana na kasi yake, uwezo wa kushindana kimwili na uzoefu wake katika soka la Ulaya.