Silva: Tumepoteza jembe

Summary


LONDON, ENGLAND. BEKI wa Chelsea, Thiago Silva amekiri hakutarajia kama Jorginho angejiunga na Arsenal dirisha la usajili la Januari lililofungwa rasmi mwezi uliopita.
Silva amesikitika na kusisitiza Chelsea imepoteza mchezaji muhimu aliyekua na mchango mkubwa hata hivyo akadai watamkumbuka kutokana na mazuri aliyotenda ndani ya klabu.

Kiungo wa kimataifa wa Italia alikamilisha uhamisho wa kujiunga na Arsenal kwa kitita cha Pauni 12 milioni na kuthibitishwa rasmi na vinara hao wa Ligi Kuu England.
Lakini kwa upande wa Silva hakupendezwa Jorginho alivyojiunga na Arsenal ambao ni wapinzani wao wenye maskani moja jijini London.
Akizungumza kwa masikitiko Silva alisema kwa namna nyingine anaelewa mambo kama haya yanatokea kwenye soka kwahiyo haina buku akubaliane na hali halisi.

"Hili ni soka ushindani mambo kama haya yantokea, alitaka kubaki England kwasababu ana familia yake hapa (London), kuna mambo mengine huwezi kuyazuia, wakati mwingine tunatakiwa kuheshimu maamuzi ya mchezaji husika, nafahamu tuna kazi kubwa mbele yetu, tumepoteza mtu muhimu na kiongozi ndani ya vymba vya kubadilishia nguo," alisema Silva
Jorginho alijiunga na Chelsea tangu mwaka 2018 akitokea Napoli kwa kitita cha Pauni 50 milioni. Jumla ya mechi alizocheza ni 213, akafunga mabao 29 na kutengeneza asisti tisa.

Sababu ya Jorginho kuondoka Chelsea ni kutokana na ukweli kwamba alikosa nafasi ya kudumu kikosi cha kwanza cha Chelsea inayonolewa na Graham Potter. Kiungo huyo alipokuwa Stamford Bridge alibeba ubingwa wa Ligi Mabingwa Ulaya Super Cup na Kombe la Dunia na ngazi ya klabu.