Sikia hii ishu ya dili la Mbappe

MADRID,HISPANIA. HABARI ndo hiyo. Real Madrid watarudi kwenye mpango wao wa kunasa saini ya Kylian Mbappe baada ya ishu ya mkataba wake huko Paris Saint-Germain kuwekwa hadharani.

Mabingwa hao wa soka wa Ufaransa walitangaza Mbappe, 23, kusaini mkataba mpya wa miaka mitatu wenye thamani ya Pauni 650,000 kwa wiki. Kwenye hilo, Mbappe alipiga picha na jezi ya PSG iliyokuwa imeandikwa namba 2025 mgongoni kwa maana ya urefu wa mkataba wake mpya, lakini sasa imefichuka mkataba wa staa huyo ni miaka miwili tu na utakwisha 2024.

Mwaka wa tatu wa mkataba huo utatokana na Mbappe mwenyewe kuamua kama anataka kubaki au kuondoka.

Kama ataamua asibaki, PSG hawatakuwa na maisha marefu ya kubaki na staa huyo zaidi ya kumpiga bei kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi ili walau wapate Pauni 150 milioni na zaidi, kuliko kubaki naye hadi 2024 na anaweza kuondoka bure itakapofika mwisho wa msimu kwa mwaka huo.

Kumekuwa na madai Mbappe alisaini mkataba huo kwa sababu tu atakapokwenda kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 awe anatokea kwenye timu inayomilikiwa na wamiliki wa kutoka Qatar kunakofanyika fainali hizo.

Fainali hizo za Kombe la Dunia zitakapomalizika, mabosi wa PSG hawatakuwa na ugumu tena wa kumzuia Mbappe asiondoke kwenye timu hiyo. Hata hivyo, kila kitu kitafanywa kwenye utaratibu mzuri isionekane kama staa huyo ameondoshwa kwenye kikosi hicho kwa sababu tu ya kulumbana na staa mwenzake, Neymar.

Kama Mbappe ataondoka basi Neymar, 30, atahesabika kama staa namba moja huko Parc des Princes. Kumuuza Mbappe ni jambo linalodaiwa litawafanya PSG kujiweka salama kwenye kanuni za Financial Fair Play (FFP).