Sesko kulamba Shilingi 500 milioni kwa wiki
Muktasari:
- Sesko, 22, aliwasili Manchester kwa ajili ya kufanya vipimo vya afya kukamilisha dili lake la Pauni 73.8 milioni akitokea RB Leipzig.
MANCHESTER, ENGLAND: BENJAMIN Sesko atajiunga na Manchester United akiwa mchezaji wa nane anayelipwa mshahara mkubwa licha ya kusajiliwa kwenda kubeba majukumu ya kuongoza safu ya ushambuliaji ya miamba hiyo ya Old Trafford.
Sesko, 22, aliwasili Manchester kwa ajili ya kufanya vipimo vya afya kukamilisha dili lake la Pauni 73.8 milioni akitokea RB Leipzig.
Straika huyo ataungana na Matheus Cunha na Bryan Mbeumo kwenye safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho cha kocha Ruben Amorim, ambacho kimepanga kurudi kivingine kwenye Ligi Kuu England msimu huu.
Sesko utakuwa usajili bora kabisa kwenye kikosi cha Man United, ambayo wengi waliamini isingekuwa kivutio kwa wachezaji wengi wa kiwango cha juu baada ya kushindwa kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita.
Na kinachoonekana Man United wala haijatumia pesa nyingi kumshawishi Sesko kujiunga kwenye timu yao badala ya kwenda Newcastle United.
Ripoti zinafichua kwamba Sesko atalipwa mshahara wa Pauni 160,000 kwa wiki huko Man United, ikiwa ni kiwango kidogo sana kutokana na mishahara mikubwa inayolipwa kwenye kikosi hicho cha Old Trafford.
Sawa, Pauni 160,000 kwa wiki ni pesa nyingi, lakini kwa kiwango hicho atakacholipwa Sesko kitamfanya kuwa mchezaji namba nane kwa mshahara. Kwa mujibu wa mtandao wa Oanda, Pauni 160,000 ni sawa na Sh532 milioni za Kitanzania.
Lakini, atakuwa kwenye nafasi kubwa ya mshahara wake kupanda hadi Pauni 200,000 kwa wiki, endapo kama Man United itafuzu tiketi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku kiwango hicho kitamfanya kuwa namba tano kwa mshahara.
Kwa mujibu wa Spotrac, Casemiro ndiye anayelipwa mshahara mkubwa kwenye kikosi cha Man United kwa sasa akipokea Pauni 350,000 kwa wiki. Kiungo Bruno Fernandes ni namba mbili, akipokea Pauni 300,000 kwa wiki.