Sesko amesema ‘yes’ Man United
Muktasari:
- Sesko, 22, amegoma kwenda kujiunga na Newcastle United, ambayo ilipeleka ofa zao mbili huko RB Leipzig kwa ajili ya kunasa huduma ya straika huyo.
LEIPZIG, UJERUMANI: STRAIKA, Benjamin Sesko ametoa jibu la 'yes' kwenye mpango wake wa kujiunga na Manchester United katika uhamisho wa dirisha hili la majira ya kiangazi.
Sesko, 22, amegoma kwenda kujiunga na Newcastle United, ambayo ilipeleka ofa zao mbili huko RB Leipzig kwa ajili ya kunasa huduma ya straika huyo.
Ofa ya pili ya Newcastle ilikuwa ya Pauni 78 milioni, ambayo klabu ya RB Leipzig waliikubali mapema wiki hii. Lakini, Newcastle ikajikuta ikishindwa tena kwenye dili hilo baada ya mchezaji mwenyewe kuwa na chaguo tofauti.
Pande zote kwenye dili hilo zinatambua wazi Sesko kipaumbele chake ni kwenda Old Trafford, kama ilivyoripotiwa na Athletic.
Man United inayonolewa na Mreno Ruben Amorim imepeleka ofa ya Pauni 73.8 milioni, ambayo imedaiwa imewashawishi mabosi wa klabu hiyo ya Ujerumani.
Makubaliano binafsi yameripotiwa kwamba hayawezi kuwa tatizo. Sesko, amekuwa kwenye rada za mabosi wa Man United, ambapo mmoja wao, anayeshughulikia usajili, anamfahamu tangu alipokuwa RB Salzburg.
Mwanzoni kulikuwa na taarifa kwamba Man United imegeukia kwa Ollie Watkins baada ya Sesko kuonekana kuikubali Newcastle, lakini Aston Villa inahitaji Pauni 60 milioni kwenye mauzo ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29. Na sasa, kibao kimegeuka, Watkins anaweza kuingia kwenye rada za Newcastle, ambayo sasa inapambana kusaka straika mpya baada ya Alexander Isak kuwaambia anataka kuondoka.
Liverpool ndiyo inayomvuruga Isak na imepeleka ofa ya Pauni 110 milioni huko St James' Park na kukataliwa, sasa ikijiandaa na ofa nyingine itakayofikia Pauni 120 milioni. Kama ilivyo kwa Sesko, Isak naye amekuwa akifanya mazoezi kivyake baada ya sasa kuwapo na timu nyingine zinazohitaji huduma zao.
Uhamisho wa Sesko kwenda Man United utafungua milango ya Rasmus Hojlund kuondoka Old Trafford, ambaye timu yake inahitaji Pauni 30 milioni tu. Sesko atakwenda kuwa sehemu mpya ya fowadi ya Man United itakayoundwa na wakali wengine walionaswa kwenye dirisha hili, Matheus Cunha na Bryan Mbeumo.