Sergio Busquets aagwa rasmi Inter Miami
Muktasari:
- Mashabiki, wachezaji na maafisa wa klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Marekani (MLS), walimuaga kwa pamoja kiungo huyo mwenye umri wa miaka 37, kabla ya mechi dhidi ya New England Revolution mapema leo Jumapili, Oktoba 05, 2025. Katika mechi hiyo New England Revolution ilikubali kichapo cha mabao 4-1.
Klabu ya Inter Miami, rasmi imemuaga kiungo wa Hispania Sergio Busquets, ambaye atastaafu soka mwishoni mwa msimu huu.
Mashabiki, wachezaji na maafisa wa klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Marekani (MLS), walimuaga kwa pamoja kiungo huyo mwenye umri wa miaka 37, kabla ya mechi dhidi ya New England Revolution mapema leo Jumapili, Oktoba 05, 2025. Katika mechi hiyo New England Revolution ilikubali kichapo cha mabao 4-1.
Kwenye uwanja wa Chase, video ya kumuenzi Busquets ilionyeshwa huku ikiwahusisha mastaa wa zamani wa FC Barcelona, akiwemo kocha wa sasa wa Manchester City, Pep Guardiola, Xavi Hernández, na Lionel Messi ambaye sasa ni mwenzake Inter Miami. Wote hawa wanajulikana kama “Core Four” wa klabu hiyo, pamoja na Luis Suárez na Jordi Alba.
Busquets ambaye alikuwa sehemu ya kikosi cha Hispania kilichotwaa Kombe la Dunia 2010, ametoa hotuba kwa hisia akiwa amezungukwa na familia yake pamoja na wachezaji wenzake wa Inter Miami.
Busquets amesema: "Sina maneno mengi. Sehemu ya moyo wangu itaendelea kubaki nanyi hapa."
Kocha wa Inter Miami, Javier Mascherano ambaye amewahi kucheza na Busquets ndani ya Barcelona, amempongeza kiungo huyo kwa kubadilisha kabisa nafasi ya kiungo mkabaji kwenye kikosi chake.
Mascherano amesema: “Kujifunza kucheza kama Busi ni vigumu, kwa sababu anachokifanya ni cha kipekee. Ni vigumu kumuiga.
“Kwa klabu hii, imekuwa ni heshima kubwa kuwa na mchezaji kama Busquets.”
Busquets alijiunga na Inter Miami Julai 2023, muda mfupi baada ya ujio wa Messi uliogeuza taswira ya klabu hiyo. Tangu wakati huo, amefanikiwa kushinda Kombe la Ligi (Leagues Cup 2023) na Supporters’ Shield 2024.