Saratani ya ubongo inavyomtesa staa NBA
Muktasari:
- Collins ameandika katika makala aliyochapisha kwenye kituo cha michezo cha ESPN, Alhamisi wiki hii amegunduliwa na glioblastoma ya hatua ya nne na kwa sasa anapokea matibabu ili kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huo ambao hauwezi kufanyiwa upasuaji.
MIAMI, MAREKANI: MCHEZAJI wa zamani wa mpira wa kikapu wa kulipwa, Jason Collins ametangaza amegunduliwa na aina kali ya saratani ya ubongo ambayo inamtesa kwa sasa.
Collins ameandika katika makala aliyochapisha kwenye kituo cha michezo cha ESPN, Alhamisi wiki hii amegunduliwa na glioblastoma ya hatua ya nne na kwa sasa anapokea matibabu ili kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huo ambao hauwezi kufanyiwa upasuaji.
Anasema uvimbe huo wa ubongo ni kama mnyama mwenye vishikio vinavyoenea chini ya ubongo wake kwa upana sawa na mpira wa baseball.
Madaktari walimwambia Collins bila matibabu, angefariki dunia ndani ya miezi mitatu.
Collins, ambaye alicheza kwa misimu 13 katika NBA, anaandika kuwa changamoto za matibabu zinafanana kwa kiasi fulani na changamoto alizokutana nazo alipokuwa uwanjani.
“Kama mwanamichezo unajifunza kutopaniki katika nyakati kama hizi,” anasema, akilinganisha matibabu hayo na kucheza dhidi ya nyota wa mpira wa kikapu Shaquille O’Neal.
“Kwangu ni kama, ‘Nyamaza na nenda ukacheze dhidi ya Shaq.’ Unataka changamoto? Hii ndiyo changamoto,” ameandika.
“Na hakuna changamoto kubwa katika mpira wa kikapu kama kucheza dhidi ya Shaquille O’Neal akiwa kileleni mwa uwezo wake na nimeshafanya hilo.”
Familia ya Collins ilikuwa imetoa taarifa fupi Septemba mwaka huu ikisema alikuwa na uvimbe wa ubongo, lakini katika makala yake anasema: “Ni wakati sasa watu wasikie kutoka kwangu moja kwa moja.”
Mwanamichezo huyo mwenye umri wa miaka 47, anaeleza saratani hiyo iligundulika baada ya kuanza kupata matatizo ya umakini.
Anafafanua jinsi alivyokosa safari ya ndege kwa sababu hakuweza kupanga mizigo yake. Baadaye, uchunguzi wa ubongo ulifichua chanzo cha matatizo yake ya umakini na kumbukumbu.
“Uwezo wangu wa kufikiri vizuri, kumbukumbu ya muda mfupi na uelewa ulitoweka, nikageuka kuwa toleo la mchezaji wa NBA la ‘Dory’ kutoka filamu ya Finding Nemo,” anatania akimrejelea samaki msahaulifu katika filamu ya Disney.
“Maisha yako yanakuwa bora zaidi unapojitokeza kama ulivyo halisi, bila hofu ya kuwa wewe mwenyewe, hadharani au faraghani. Huyu ni mimi. Hili ndilo ninapitia,” anasema.
Kwa sasa Collins anatibiwa kwa kutumia dawa iitwayo Avastin ili kupunguza kasi ya ukuaji wa uvimbe huo na amekuwa akisafiri kwenda Singapore kwa ajili ya aina maalum ya tiba ya kemotherapi inayolenga moja kwa moja uvimbe.
Anaandika kuwa anatumaini matibabu yake yatachangia kuendelezwa kwa njia bora zaidi za kupambana na ugonjwa huo, na anaweza kuongoza kwa mfano.
Collins ambaye ni mzaliwa huyo wa California, alichezea timu sita katika misimu yake 13 ya NBA. Hapo awali aliwahi kuorodheshwa katika orodha ya watu 100 wenye ushawishi mkubwa zaidi duniani ya jarida la Time. Alistaafu mwaka 2014.