Ruben Amorim sasa achanganyikiwa
Muktasari:
- Baada ya kipa wake namba moja raia wa Cameroon, Andre Onana kuumia, Amorim sasa anaangalia uwezekano wa kusajili kipa mwingine atakayesimama langoni.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim kichwa kinauma. Katika dirisha hili Mreno huyo alikuwa na mpango wa kujenga upya kikosi chao kwa kusajili maeneo muhimu kama ushambuliaji, mabeki na viungo lakini sasa mambo yameenda tofauti.
Baada ya kipa wake namba moja raia wa Cameroon, Andre Onana kuumia, Amorim sasa anaangalia uwezekano wa kusajili kipa mwingine atakayesimama langoni.
Awali, Onana pia alikuwa katika hesabu za kuuzwa ili zipatikane pesa zitakazosaidia usajili lakini kutokana na jeraha alilopata hata mpango huo umekufa na itailazimu timu kuchukua pesa katika bajeti iliyopanga kutumia kufanya usajili wa maeneo mengine.
Kipa huyo namba moja amepata maumivu ya msuli wa paja (hamstring) ambayo yanatarajiwa kumweka nje na kukosa mechi za mwanzoni mwa msimu.
Onana mwenye umri wa miaka 29 amekuwa na kipindi kigumu tangu alipojiunga na United kutoka Inter Milan mwaka 2023 kwa ada ya takribani pauni 50 milioni na amekuwa akishambuliwa vikali kwa makosa kadhaa makubwa aliyoyafanya msimu uliopita.
Kwa mujibu wa tovuti ya The Telegraph, Man United ina wasiwasi kuwa Onana atakuwa nje kwa wiki sita hadi nane, hali itakayomfanya kuukosa mchezo wao wa kwanza wa msimu dhidi ya Arsenal utakaopigwa Agosti 17.
Hata hivyo, anatarajiwa pia kusafiri kwenye ziara ya maandalizi ya msimu huko Marekani lakini hatacheza mechi yoyote.
Ripoti zinaeleza Amorim sasa anaangalia uwezekano wa kumsajili kipa mpya, licha ya uwepo wa Altay Bayindir, Radek Vitek na Tom Heaton katika kikosi.
Mechi za maandalizi ya msimu kwa Man United zitaanza Julai 19 ambapo itacheza dhidi ya Leeds United huko Stockholm, Sweden. Baadaye itasafiri hadi Marekani kwa ajili ya mechi dhidi ya West Ham, Bournemouth na Everton kabla ya kurejea nyumbani kucheza na Fiorentina. katika dimba la Old Trafford, Agosti 9.