Ruben Amorim aitwa Brazil
Muktasari:
- Amorim amekuwa hana kazi tangu alipoondoka Manchester United mwezi uliopita baada ya kufukuzwa na mashetani wekundu hao kutokana na mfululizo wa matokeo yasiyoridhisha.
RIO DE JANEIRO, BRAZIL: VIGOGO wa soka nchini Brazil, Vasco da Gama, wanaripotiwa kuwa katika mazungumzo na kocha Ruben Amorim ili kumwajiri awe kocha wao mpya.
Amorim amekuwa hana kazi tangu alipoondoka Manchester United mwezi uliopita baada ya kufukuzwa na mashetani wekundu hao kutokana na mfululizo wa matokeo yasiyoridhisha.
Inaelezwa pia aligombana na viongozi wa klabu hiyo baada ya kusema kwamba hakufurahishwa na yaliyokuwa yakiendelea nyuma ya pazia.
Baada ya kuondoka kwake, Michael Carrick aliteuliwa kuwa kocha wa mpito wa hadi mwisho wa msimu na sasa
anaonekana kuwa katika rada za Vasco da Gama.
Klabu hiyo ya jijini Rio de Janeiro iko katika harakati za kutafuta kocha mpya baada ya kuondoka kwa Fernando Diniz wiki iliyopita.
Diniz alifutwa kazi na Vasco Jumapili kufuatia kipigo cha 1-0 kutoka kwa Fluminense. Kwenye ligi, klabu hiyo inashika nafasi ya 17 katika msimamo ikiwa imepata pointi moja tu katika mechi tatu zilizopita.
Inaelezwa kuwa Vasco, kwa sasa wanampa kipaumbele kocha wa Al-Rayyan, Artur Jorge. Hata hivyo, Amorim pia bado yupo kwenye orodha yao ya makocha inaowafuatilia.
Kocha huyo raia wa Ureno aliiongoza Manchester United katika mechi 63 ndani ya kipindi cha miezi 14. Katika kipindi hicho alipata ushindi mara 25, sare 15 na kupoteza 23.
Kabla ya Man United, Amorim aliwahi kuzinoa timu kadhaa za Ureno ikiwa pamoja na Sporting Lisbon na Braga.