Ronaldo: Mwanangu hatukubali mimi na Messi
Muktasari:
- Ronaldo na Messi wametawala anga la soka kwa muda mrefu wakicheza kwa kiwango bora wakiwa Hispania na kijumla wamechukua tuzo 13 za Ballon d'Or.
RUYADH, SAUDI ARABIA: NDO hivyo. Staa wa Al Nassr, Cristiano Ronaldo amefichua mtoto wake Mateo, kuna mchezaji mmoja tu anayekumbali duniani ambaye sio yeye wala mpinzani wake wa muda mrefu Lionel Messi.
Ronaldo na Messi wametawala anga la soka kwa muda mrefu wakicheza kwa kiwango bora wakiwa Hispania na kijumla wamechukua tuzo 13 za Ballon d'Or.
Ubora wao umesababisha kuwepo kwa mashabiki wa makundi mawili wale wanaomshabikia Ronaldo na Messi lakini mambo yamekuwa tofauti katika familia ya Ronaldo ambako watoto wake wanaamini Kylian Mbappe ndiye mchezaji bora zaidi.
Katika mahojiano yake na tovuti ya La Sexta, Ronaldo ameelezea jinsi anavyochekwa na mtoto wake, Mateo ambaye anaamini Mbappe ndiye bora zaidi kuliko yeye.
"Mateo, anampenda sana Kylian Mbappe. Wakati mwingine ananiambia: ‘Hey baba, Mbappe ni bora kuliko wewe,’ na mimi namjibu kwa kusema: ‘Hapana, mimi ni bora kuliko yeye, nimefunga mabao mengi zaidi."
Ronaldo ambaye kwa sasa anapambana kufikisha mabao 1000 baada ya kufikisha 900 mwishoni mwa mwaka jana, nyayo zake zinafuatwa vizuri na Mbappe ambaye ameanza kung'aa akiwa na Real Madrid aliyojiunga nayo dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana.
Akiwa na Al Nassr ambayo anamaliza nayo mkataba mwisho wa msimu huu amecheza mechi 23 za michuano yote na kufunga mabao 20.