Ronaldo awekwa mkeka tena
Muktasari:
- Nyota huyo wa zamani wa Manchester United, mwenye umri wa miaka 41, anadaiwa kukasirishwa na kiwango cha matumizi ya klabu yake ikilinganishwa na wapinzani wao baada ya kutofanya usajili wa maana kwenye dirisha la usajili la Januari.
RIYADH, SAUDI ARABIA: SUPASTAA, Cristiano Ronaldo ameondolewa kwenye kikosi cha siku ya mechi cha Al-Nassr kwa mara ya pili mfululizo baada ya kuingia kwenye mgomo.
Nyota huyo wa zamani wa Manchester United, mwenye umri wa miaka 41, anadaiwa kukasirishwa na kiwango cha matumizi ya klabu yake ikilinganishwa na wapinzani wao baada ya kutofanya usajili wa maana kwenye dirisha la usajili la Januari.
Inaripotiwa Ronaldo alikataa kucheza kwenye mechi ya timu yake, ambapo hakuhusika kwenye ushindi wa 1-0 dhidi ya Al-Riyadh, Jumatatu iliyopita. Kulikuwa na matumaini kutoka kwa maofisa wa klabu kwamba angerudi baada ya onyo kali kutoka kwa Ligi Kuu Saudia (Saudi Pro League). Hata hivyo, Ronaldo hakuonekana kabisa baada ya kocha Jorge Jesus kutangaza kikosi chake kwa pambano kubwa la Al-Nassr dhidi ya wapinzani wao Al-Ittihad.
Kocha huyo aliwajumuisha washambuliaji Kingsley Coman, aliyewahi kuichezea Bayern Munich, pamoja na mkali wa zamani wa Liverpool na Bayern pia, Sadio Mane na aliyekuwa fowadi wa Atletico Madrid na Chelsea, Joao Felix.
Klabu haikutaja chochote maalumu kuhusu nahodha wao na mchezaji nyota wakati wa kutangaza kikosi cha kwanza kwenye mitandao ya kijamii.
Ripoti zilidai kuwa Ronaldo alitarajiwa kurejea klabuni Ijumaa kuelekea mchezo huo. Sky Sports iliripoti kuwa maafisa walikuwa na imani kwamba angemaliza mgomo wake na kucheza dhidi ya Al-Ittihad.
Ronaldo amekuwa muhimu sana kwenye kikosi cha Al-Nassr msimu huu, akifunga mabao 17 na akishindwa kufunga katika mechi nne pekee. Hata hivyo, alipewa onyo kali na Ligi Kuu ya Saudi kwamba hata mchezaji wa hadhi yake hakuwa mkubwa kuliko ligi yenyewe baada ya kuchukua msimamo wake.
Ligi ilitoa taarifa Alhamisi iliyopita ikisema: “Ligi Kuu ya Saudi imejengwa juu ya kanuni rahisi: kila klabu inafanya kazi kwa uhuru chini ya sheria zilezile. Kila klabu ina bodi yake, wakurugenzi wake na uongozi wake wa soka. Uamuzi kuhusu usajili, matumizi ya fedha na mkakati hufanywa na klabu husika, ndani ya mfumo wa kifedha ulioundwa kuhakikisha uendelevu na ushindani wa haki.
"Mfumo huo unatumika kwa kila klabu. Cristiano amekuwa akihusika kikamilifu na Al-Nassr tangu alipojiunga na amecheza jukumu muhimu katika ukuaji na malengo ya klabu. Kama mshindani wa hali ya juu, anataka kushinda. Lakini hakuna mtu mmoja, haijalishi ana umuhimu gani anayefanya maamuzi nje ya mamlaka ya klabu yake mwenyewe. Shughuli za hivi karibuni za usajili zinaonyesha wazi uhuru huo. Klabu moja iliimarika kwa njia fulani. Klabu nyingine ilichagua mkakati tofauti. Hayo yalikuwa maamuzi ya klabu, yaliyofanywa ndani ya vigezo vya kifedha vilivyoidhinishwa.”
Ronaldo ameibadilisha kwa kiasi kikubwa Ligi Kuu ya Saudi tangu alipojiunga na Al-Nassr mwaka 2022 ambapo anaripotiwa kulipwa Pauni 488,000 kwa siku.