Ronaldo anabipu watu wanampigia
Muktasari:
- Ronaldo, mwenye umri wa miaka 41, hajacheza katika mechi mbili za mwisho za Al-Nassr baada ya kile kinachoonekana kama kugoma kimya kimya, akionyesha kutoridhishwa kwake na Mfuko wa Uwekezaji wa Umma wa Saudi Arabia (PIF) kwa kile anachodai ni kuzipendelea klabu pinzani katika shughuli za usajili wa wachezaji wa maana.
RIYADH, SAUDI ARABIA: AL-Nassr hawatamzuia Cristiano Ronaldo iwapo nyota huyo mwenye hasira ataamua kushikilia msimamo wa kuondoka wakati wa dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi, huku kipengele cha kuvunja mkataba cha Pauni 43 milioni kilichopo kwenye mkataba wa nahodha huyo wa Ureno kikitarajiwa kuanza kutumika mwishoni mwa msimu.
Ronaldo, mwenye umri wa miaka 41, hajacheza katika mechi mbili za mwisho za Al-Nassr baada ya kile kinachoonekana kama kugoma kimya kimya, akionyesha kutoridhishwa kwake na Mfuko wa Uwekezaji wa Umma wa Saudi Arabia (PIF) kwa kile anachodai ni kuzipendelea klabu pinzani katika shughuli za usajili wa wachezaji wa maana.
Baada ya kukosa mechi ya Ijumaa, dhidi ya Al-Ittihad, tetesi kwamba Ronaldo anaweza kuondoka kwenye Ligi Kuu ya Saudia zimezidi kushika kasi na inaelezwa kuwa viongozi wako tayari kukata kabisa mahusiano na gwiji huyo wa zamani wa Manchester United na Real Madrid.
Kwa mujibu wa ripoti ya The i Paper, maafisa wa Saudia wameshtushwa na mwenendo wa Ronaldo na wameshikilia msimamo kwamba hakuna mchezaji aliye juu ya malengo yao kwa ajili ya ligi hata kama ni mshindi mara nyingi wa Ballon d’Or.
Kutokana na hilo, wako tayari “kumsajili mfalme mpya” iwapo Ronaldo, ambaye amekuwa uso wa ligi hiyo tangu ajiunge nayo Desemba 2022, ataondoka. Chanzo cha karibu na ligi kililiambia jarida hilo: “Kwa kuwa majina makubwa mengine yanaondoka, tutaangalia wachezaji wengi wakubwa majira ya joto. Mohamed Salah na Bruno Fernandes wangekuwa chaguo kamili. Salah hasa, kwa sababu angevutia zaidi mashabiki Waarabu kutokana na kuwa Muislamu.” Ingawa Manchester United haina nia ya kumrudisha Ronaldo Old Trafford kwa mara ya tatu, bado kuna uwezekano mshambuliaji huyo kurejea kwenye klabu yake ya kwanza, Sporting Lisbon.