Riise amtaka Isak Anfield
Muktasari:
- Kocha Arne Slot amemkosoa Nunez kwa kukosa umakini baada ya straika huyo wa Pauni 85 milioni kupoteza nafasi ya wazi ya kufunga bao la ushindi kwenye sare ya 2-2 dhidi ya Aston Villa, Jumatano iliyopita.
LIVERPOOL, ENGLAND: MABOSI wa Liverpool wameshauriwa kufungua pochi kumsajili straika wa Newcastle United, Alexander Isak kwenda kuchukua mikoba ya Darwin Nunez ambaye hana maajabu tangu alipotua Anfield.
Kocha Arne Slot amemkosoa Nunez kwa kukosa umakini baada ya straika huyo wa Pauni 85 milioni kupoteza nafasi ya wazi ya kufunga bao la ushindi kwenye sare ya 2-2 dhidi ya Aston Villa, Jumatano iliyopita.
“Ningetamani afunge pale, lakini kama unavyojua ile ni nafasi tu na nafasi si asilimia 100 kwamba kuna uhakika mpira utaninga nyavuni na wachezaji wamekuwa wakikosa nafasi,” alisema Slot.
“Ile sikubaliani nayo, lakini ni ngumu pia kukubaliana na ishara yake baada ya kukosa nafasi ile. Nadhani ile ilipaswa kumwingia akilini, lakini hakuonekana kuwa tayari kusaidia timu, hicho kitu lazima tukizungumze.”
Lakini, Nunez, ambaye alikuwa kwenye rada za klabu za Saudi Arabia dirisha lililopita la majira ya baridi huenda asiwe na chochote cha kumthibitishia Slot, hasa baada ya beki wa zamani wa Liverpool, John Arne Riise kusema timu hiyo inapaswa kuingia vitani na Arsenal na Chelsea kumfukuzia Isak, ambaye anaripotiwa saini yake inaweza kugharimu Pauni 150 milioni. “Tumesikia uvumi mwingi ukisema kwamba naye atakuwa tayari kwenda kujiunga na Liverpool. Kila straika atapenda kwenda kucheza Liverpool, nadhani utakuwa usajili mzuri,” alisema Riise.